2014-09-18 08:17:46

Makatekista -Injilisheni kuanzia ndani ya familia zenu


Semina ya makatekista wa Jimbo la Roma imemalizika Jumanne 16 Septemba, katika Jimbo la Roma kwa ajili ya kuwaandaa Makatekista katika ufundishaji wa elimu ya dini Parokiani, juhudi mpya za kitume zinazo anza hivi karibuni baada ya likizo ya miezi mitatu ya kiangazi.

Ni utume wa kanisa kwa watoto na vijana kupokea mafundisho msingi ya kanisa wakiwa wadogo na kuendelea. Katika semina hiyo, wazo kuu limekuwa ni kuangalia upya mbinu za kuinjilisha vijana, kwa kuanza katika familia zao. Makatekista wameombwa kuwa na imani kuu kwa Mungu inayochotwa kutoka Injili, ili iwape mwanga wa kuachanganua maisha yao.

Pia makatekista waliombwa kuwa na elimu zaidi, kwani itawasadia katika kukabiliana na vijana watakaokutana nao katika parokia na kuweza kuwasaidia katika changamoto zao na kuwapa uhusiano mzuri na matumaini.

Na katika kufunga semina hiyo ya makatekista, Kardinali Agustino Vallini Decano wa Dekania ya Roma alisema, ili kuweza kugusa moyo wa kijana wa leo, inahitaji upendo mkuu kwani vijana wa siku hizi wako tofauti kulinganisha na kizazi kilichopita katika hali zote, mabadiliko yanayotokana na changamoto wanazokutana nazo , hivyo hakuna maana ya kupunguza mafunzo ya katekisimu wanapofika kwenye mafunzo hayo , maana mafunzo haya ndiyo msingi, ndiyo chemichemi .

Inahitaji kuwajibika kwani ni utume mkubwa na parokia ndiyo sehemu muhimu ya kupokea habari njema na kupeleka habari njema kwa vijana na kwa familia zao , ambazo kwa nyakati hizi imani inaelekea kuyumbayumba.

Naye Pia Mkurugenzi wa ofisi ya Katekesi Jimbo la Roma Padre Andrea Lonardo, aliwakumbusha maneno ya Papa Fransisko anavyosistiza juu ya parokia, kwani inapaswa kuwa karibu na watu, na watu vilevile waonekane katika parokia, isiwe tabia ya watu kuonekana wakati wa misiba, ubatizo au kupokea kumunyo ya kwanza.

Vilevile alisema kwamba, Papa anapenda kuona Parokia zinapaswa kufunguliwa kupokea watu wote bila mipaka. Na Parokia zinapaswa zitoke nje kuangalia watu wanoteseka na matatizo mbalimbali ya kimwili na kiroho, sehemu zenye matatizo ya elimu, matatizo ya wagonjwa , wasio kuwa na mtu wa kuwaangalia , walemavu katika hali zote.

Kuna matatizo ya vijana wengi wanapomaliza kupokea kumunio Takatifu ya kwanza wanapotea, na hivyo ni famila ambazo inabidi zigundue kwa upya uzuri wa kuwa na imani kwa Mungu,na pia familia zinapswa zionyeshe mifano ya imani kwa Mungu kwa watoto wao.Kwani katika ujana mambo ya utoro kanisani hayakosekani na hivyo ni muhimu kwa wazazi kuwasindikiza watoto wao kaika njia za makuzi ya vijana hasa kutembea ndani ya Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.