2014-08-23 09:51:11

Roho ya kwanini chanzo cha chuki na uhasama katika Jamii


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Kwa mara nyingine tena tujumuike katika kipindi chetu hiki, hasa kwa wakati huu tunapoitazama familia kama shule ya fadhila mbalimbali na kwa ujumla wake kama shule ya maadili. RealAudioMP3

Katika kipindi kilichopita tulihekimishana juu ya kupenda kusema ukweli. Kuepuka na kuzuia kabisa tabia ya kusema uongo, kwani uongo huharibu kabisa amani kati ya watu, uongo huangamiza, uongo huua.

Leo hii, mpendwa msikilizaji ninakualika tena tutafakari juu ya vilema vingine viwili vinavyoendana na uongo, navyo si vingine bali ni uchongezi na uchonganishi. Uchongezi ni nini? Ni tabia ya mtu mwenye akili timamu na utashi, kusema mabaya ya mtu kwa watu wenye mamlaka kwa nia ya kudhuru. Mchongezi huwa hana jema, huwa na nia mbaya ya kutaka kumdhuru huyo anayemchongea. Na mchongezi hupeleka habari mbaya ya mtu kwa mtu ambaye anaamini kuwa atatoa madhara. Ndiyo maana tumesema ni tabia ya mtu mwenye akili timamu na utashi; kwa sababu anajua anachotenda, anajua namna anayotenda na anajua pia matokeo ya anachokisema.

Sisi tunatazama uchongezi kama tabia mbaya sana, tena imewadhuru wengi. Katika kipindi hiki tunataka tudhamirishane hivi, ili kila mmoja ajibidishe kuiepa tabia ya uchongezi (na uchonganishi). Na maandiko matakatifu yanalaani tabia ya uchongezi, uchongezii ni kama uangamizi mkuu.

Neno linasema “alaaniwe mtu mchongezi na mdanganyifu, maana amewaangamiza wengi wanaoishi kwa amani. Uchongezi umevunja amani ya watu wengi...uchongezi umeangamiza miji yenye nguvu. Uchogezi umewafanya wake waaminifu wawakimbie waume zao, na kuwanyang’anya matunda ya jasho lao....Yeyote anayemsikiliza mchongezi hatatulia moyoni, wala hataishi kwa amani. Pigo la mijeledi hubakiza kovu, lakini pigo la ulimi huvunjavunja mifupa. Watu wengi wameuawa kwa upanga, lakini ni wengi zaidi waliouawa kwa ulimi. Kifo kiletwacho na uchongezi ni kibaya, kuzimu ni afadhali kuliko uchongezi” (YbS 28: 13-21).

Uchonganishi ni tabia ya kupandikiza chuki kati ya watu. Mtu mwenye tabia ya uchonganishi, hulenga kuondoa amani, furaha na maelewano mema kati ya watu. Na mwingine katika uchonganishi huohuo hulenga kuendeleza moto wa chuki kati ya wagombanao. Uchonganishi au ufitanishi huweza kuwa na msingi wenye ukweli, lakini mara nyingi ni tanzu za uongo. Maandiko yanatuambia uchonganishi ni kati ya mambo machukivu sana mbele za Bwana.

Neno linasema “kuna vitu sita anavyovichukia Bwana, naam vipo saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, mikono imwagayo damu, moyo uwazao mawazo mabaya, miguu myepesi kukimbilia maovu, shahidi wa uongo, naye apandaye mbegu ya fitina kati ya ndugu” (Mith. 6:16-19).

Asili ya uchonganishi na uchongezi ni roho mbaya. Roho ya kutaka na kupenda kuharibu amani za watu, kuharibu kazi za watu, kuharibu maendeleo ya watu, na kuchafua majina ya watu wasafi. Na tukichunguza ndani zaidi ya tabia hii, tutakuta kuna wivu unaobeba tabia ya kusema wakose kabisa au tukose wote. Kwa ujumla wake, uchonganishi na uchongezi ni tabia haribifu sana.

Wimbo wetu hapa tunaupeleka katika Kanisa la nyumbani. Watoto wetu wafundishwe unyoofu, wanidhamishwe katika kusema ukweli, na wawe na ujasiri wa kuambiana ukweli. Watoto wakiwa wanachongeana chongeana kwa wazazi, na wazazi wakikaa kimya, basi tabia hiyo huendelea na kukomaa sana kwa watoto, wanakua nayo hivyo na wanendelea nayo hadi mashuleni, na baadaye hata maofisini wanakuwa sio wachongezi tu, bali wafitanishi hodari. Ofisi ikiingiliwa na mtu mchongezi, basi hapo usalama hamna. Wapo watakaodhurika vibaya kwa tabia ya uchongezi. Wapo pia walioachishwa kazi pasipo haki, kwa sababu tu mchongezi alipewa nafasi.

Tabia ya mtu ukubwani, huwa na msingi katika malezi ya utotoni. Familia zetu zina umuhimu sana katika kuunda watu wenye kufaa katika jamii. Dalili za tabia ya ukubwani kwa kiasi kikubwa huonekana tangu udogoni. Ndio maana daima twawalilia wazazi na walezi, kuweni karibu na watoto, someni vijitabia vyao visivyofaa na kujitahidi kiviyeyusha mapema, kwani wanasema, Samaki mkunje angali mbichi.
Tunahitimisha kipindi chetu kwa kutoa rai ya jumla kwetu sote, tulio wachongezi na wachonganishi, tuache kwani ni chukizo kwa Bwana nasi wenyewe hutuletea aibu baadaye.

Mpendwa msikilizaji, kila mmoja katika utu uzima anajifahamu! Basi na tujibidishe sana kukomesha vilema vyetu vya roho na mwili, na neno la Mungu lituongoze. Neno linasema, “Maandiko matakatifu yote yameandikwa kwa uongozi wa Roho Mtakatifu, na yanafaa kwa kufundisha ukweli, kuonya, kusahihisha makosa na kuwaongoza watu waishi maisha adili” (2Tim.3:16).

Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.