2014-08-23 12:22:55

Mshikamano wa kiekumene katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji


Baraza la Makanisa Ulimwenguni kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 5 Septemba, 2014 litafanya semina kwa ajili ya viongozi wa Kanisa, itakayoongozwa na kauli mbiu “Tathmini ya ya taalimungu ya kiekumene kwa ajili ya viongozi wa Makanisa ya wahamiaji”.

Semina hii itafanyika kwenye Chuo cha Kiekumene cha Bossey, kilichoko nchini Uswiss. Hii itakuwa ni nafasi kwa viongozi wa Makanisa kuonesha mshikamano kwa kuwa wamoja. Semina hii itahudhuriwa pia viongozi wa mashirika ya kiraia.

Washiriki hawa wanatoka hususan nchini Sierra Leone, Nigeria, Togo na Guyana, lakini ni viongozi wanaowahudumiwa wakimbizi na wahamiaji wanaoishi Barani Ulaya. Dr. Amèlè Ekuè, mratibu wa semina hii anasema kwamba, uhamiaji ni kati ya changamoto za kimataifa kwa nyakati hizi, kwani kuna watu wanalazimika kuzikimbia au kutafuta maisha bora zaidi ughaibuni kutokana na na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, dhuluma na nyanyaso.

Ni watu wanaohitaji ulinzi na haki zao kuthaminiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Ongezeko la makundi makubwa ya wahamiaji na wageni, imekuwa ni fursa ya ujenzi wa mshikamano wa kiekumene anasema Mama Ekuè.

Umefika wakati wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kuiangalia changamoto hii, kumbe wakati wa semina kwa viongozi wa wahamiaji mambo kadhaa yatajadiliwa. Hii ni pamoja na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi yao kuhusu hali ya wahamiaji, changamoto zilizopo, mafanikio na matatizo katika utume wao miongoni mwa wahamiaji na wakimbizi katika Makanisa yao. Wajumbe wataangalia mikakati inayoweza kuboresha taalimungu ya kiekumene kuhusu utume wa Makanisa miongoni mwa wa wahamiaji.








All the contents on this site are copyrighted ©.