Mabadiliko katika sekta ya afya Nigeria hayalengi kudumisha zawadi ya uhai
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria halikuridhishwa sana na muswada wa sheria uliopitishwa
Bungeni hivi karibuni kuhusiana na masuala ya afya hata baada ya kufanyiwa marekebisho
ya msingi, ili kuhakikisha kwamba, wananchi wote wa Nigeria wanapata tiba makini hospitalini
bila ubaguzi.
Maaskofu Katoliki Nigeria wanasema muswada huu wa sheria licha
ya uzito wake kwa masihai ya wengi, lakini bado kuna vipengele vinavyotishia usalama
wa haki ya maisha. Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria,
akizungumzia kuhusu muswada huu anasema vipengele namba 50, 51 na 52 vinahusika zaidi.
Wafanyakazi katika sekta ya afya pia wameonesha wasi wasi wao kuhusiana na
kipengele namba 50 kinachogusia utoaji wa viini tete na masuala mengine ya kimaadili,
yanayoweza kupelekea baadhi ya watu kuanza kujiingiza katika biashara haramu ya viungo
vya binadamu. Maaskofu wanamshauri Rais Goodluck Jonathan kutia sahihi muswada huu
baada ya kufanyiwa marekebisho msingi.
Mabadiliko katika sekta ya afya ni mambo
ambayo yamejadiliwa kwa miaka mingi bila mafanikio. Takwimu za Shirika la Afya Duniani
zinazonesha kwamba, umri wa wastani wa mtu kuishi nchini Nigeria ni miaka 54. Vifo
vya watoto wadogo na wanawake wajawazito bado viko juu sana. NI wanawake asimilia
3% wenye virusi vya Ukimwi ambao wanapata dawa za kurefusha maisha.