Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 21 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa
Mwamini mwana wa Mungu unayetegea sikio Radio Vatican, Tumsifu Yesu Kristo. Tunakuleteni
tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 21 mwaka A tukiongozwa na Nabii Isaya, Mtume
Paulo na Mwinjili Matayo, ambao wanatuambia kuwa imani thabiti katika Yesu Kristo
Mwana wa Mungu ni msingi wa wokovu wetu.
Nabii Isaya
katika somo la kwanza anatoa mafundisho yake wakati wa utawala wa Hezekia, yaani wakati
wa utawala huu aliyekuwa mtunza mfuko anatumia vibaya mali aliyokabidhiwa yaani hajali
shida za watu. Anajitazama yeye binafsi, anajiimarisha katika utajiri binafsi na anakuza
jina lake.
Ni kwa shida hii Nabii Isaya anafundisha kinyume na madhulumu yanayofanywa
na wenye madaraka. Anawaambia kuwa watanyanganywa funguo na watakabidhiwa wengine
wenye kushika sheria ya Bwana. Funguo ni alama ya madaraka, ni alama ya utawala na
hivi nabii anawaambia kuwa madaraka yenu yatapokonywa na Mungu. Mpendwa msikilizaji,
ndiyo kusema hivi leo kuna wenye mamlaka wengi ambao wamejiimarisha katika mali, katika
ubaya, kiasi kwamba wanapopita mitaani petu wanajionesha katika sura hiyo! Wanatoa
harufu ya dhuluma.
Nabii anawaonya kuacha mali hizo na kumrudia Bwana. Hata
hivyo tukumbuke kuwa Mungu hachukizwi na mali bali na tunaweza kuwa na mali na madaraka
halali kama vitu hivi vinatupatia nafasi ya kuwaongoza wengine vema tukiwajalia haki
na ustawi wa maisha yao.
Mtume Paulo anatualika kutambua mara na kuacha ubaya
tukiongozwa na hekima ya Mungu ambayo inapita ufahamu wa kibinadamu. Kwa jinsi hiyo
hatuna budi kuitafuta na kuipokea hekima ya Mungu ili itusaidie katika kutawala taifa
la Mungu na mali tulizokabidhiwa na Mungu mwenyewe. Mtakatifu Paulo anazidi kutuambia
jinsi hekima ya Mungu ilivyo ya ajabu ya kwamba katika ubaya wa Wayahudi yaani wanapomkataa
Masiha, mara moja milango inafunguka kwa ajili ya mataifa ndiyo sisi! Hakika hekima
yake haichunguziki, hatuna uwezo wa kuielewa vema kumbe yafaa kusadiki na kujiweka
katika maongozi ya Mungu. Ndiyo kusema katika udhaifu wetu Mungu aweza kuibua jambo
la ajabu kwa ajili ya wokovu wetu.
Mwinjili Mathayo anatuletea Kristu aliye
katika harakati za uchungaji, yuko Kaisaria Filipi, yuko katika kutekeleza utume wake
uliomleta duniani. Huko anataka kuhakiki kama watu na mitume wanamfahamu kina au bado.
Anaweka swali mbele ya mitume, Je watu wasema mimi ni nani? Na ninyi mwasema mimi
ni nani? Jibu toka jumuiya ya watu ni kwamba Yesu ni mmojawapo wa manabii, ni Ni nabii
Eliya, ni Yohane Mbatizaji na mwishoni jibu la Mitume linatolewa na Mtakatifu Petro
akisema “wewe ndiye Kristo, mwana wa Mungu aliye hai” Jibu hili la Mtakatifu Petro
ndilo linabeba kiini cha injili, ni ufunuo wa Masiya mpakwa mafuta wa Bwana.
Kwa
njia ya jibu hili mwinjili Mathayo anataka watu wote wamjue Kristo kama masiya na
hakuna tena mfalme mwingine zaidi yake. Watu walitoa jibu kuwa ni nabii lakini sasa
mwinjili anatuambia wakati wa manabii umekwisha na hivi ni Kristo pekee mwana wa Mungu
aliye hai. Mpendwa hivi leo ukiulizwa Yesu ni nani utasema nini? Kwangu mimi Kristu
ni mkombozi wa maisha yangu anayenipenda katika udhaifu wangu, anayeniita kila siku
kutubu na kumrudia yeye kwa njia ya kitubio. Ni yule anayewapenda wote bila ubaguzi
maskini kwa matajiri.
Tupige hatua kidogo mbele katika tafakari yetu tuone
je jibu la Mt Petro linaishia pale tu au lina matunda? Jibu la Mtakatifu Petro lina
matokeo makubwa mno, Mtakatifu Petro atakuwa mwamba ambapo Kanisa la Kristu litajengwa.
Na si mwamba tu bali ni mwamba wa kujengea, ni mwamba wa imani. Makatifut Petro amekiri
imani ambayo lazima ikue na izae matunda. Mwamba huu ni imara na hivi hata nguvu za
kuzimu haziwezi kuubomoa. Anakabidhiwa funguo ambazo tulisikia Nabii Isaya akizungumzia
kwamba mtunza hazina atanyanganywa na Bwana. Tunarudia tena kusema kuwa funguo ni
alama ya madaraka, uwezo juu ya taifa la Mungu.
Oneni mpendwa, ni mamlaka
gani Mtakatifu Petro amepewa ili ailinde imani! Asimamie Kanisa, afundishe, aonye
na zaidi aimarishe imani ya waamini wote wa taifa la Mungu. Leo hii wajibu huu anao
Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu wa Roma na mchungaji mkuu wa Kanisa
lote la ulimwengu. Tunao wajibu wa kumwombea ili imani yake ibaki imara na abaki katika
kuhudumu na kusimamia taifa takatifu la Mungu akijiimarisha katika imani na umisionari.
Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.