2014-08-21 10:30:36

Leo ni kiti moto patashika nguo kuchanika!


Waandishi wa Habari ni hodari sana wa kutafuta habari na kuzitangaza katika vyombo vya habari. Namna yao ya kuhoji habari waswahili wanaiita “Kumweka mtu kiti moto.” Wanao ufundi wa kumweka mtu kiti moto. Mbele ya Mungu, binadamu tunalinganishwa na waandishi wa habari.

Tunamweka Mungu kiti moto kwa kumhoji maswali mengi yatokanayo na hali halisi ya maisha tunayokabiliana nayo, kuhusu mateso, njaa, kiu, mauaji, uonevu, dhuluma, magonjwa nk.

Katika Agano la kale waisraeli walimwuliza Mungu maswali mengi sana. Katika Agano Jipya kadhalikaYesu aliwekwa kiti moto na Wafarisayo, Waandishi wakuu na Makuhani, hata na raia wenzake wakimhoji: “Wewe ni nani? Umetoka wapi? unafundisha kwa mamlaka ya nani? Kwa nini wanafunzi wa Yohane na Mafarisayo wanafunga lakini wafunzi wako hawafungi? Licha ya Yesu kujionesha alivyo na anavyotenda, waliendelea tu kujihoji “ni nani huyu anayefukuza mashetani, anayeponya wagonjwa, anayewafufua wafu?”

Leo Yesu anatugeuzia kibao anatuweka sisi kiti moto akiwa na lengo la kutufundisha namna nzuri ya kuhoji habari na kupata majibu yenye tija. Yesu anahoji maswali mawili tu ya msingi: Mosi, “Watu wananionaje? Pili, “Ninyi wenyewe mnanionaje?” Maswali hayo yanadai majibu ya dhati siyo ushabiki. Lengo lake ni kujiandika ndani yako ili uwe gazeti na watu waweze kumsoma katika wewe.

Swali la kwanza linahoji jinsi watu wengine wavyomwona na wanavyoziona sera zake za maisha. “endapo tunaweza kuzilinganisha sera zake na za watu wanaojulikana kuwa ni wa pekee hapa duniani,” yaani matajiri, watu wanaoheshimika sababu ya mali. Aidha, tunaweza kumlinganisha Yesu na mtu wa dini kama walivyokuwa makuhani wa enzi zake, wenye hadhi ya utakatifu au wasomi waliobobea katika ya elimu dunia?

Wanafunzi wa Yesu wanatuwakilisha kujibu swali hilo la kwanza kwa sababu wamerudi hivi karibu toka kijijini walikokuwa wanawahudumia watu. Hao walimwingiza Yesu katika mlolongo wa manabii maarufu. Sera zao zilihusu maisha ya haki, ya ukweli; juu ya imani kwa Mungu kweli, na jinsi bora ya kuhusiana na huyo Mungu.

Nabii wa kwanza wanayemlinganisha na Yesu ni Yohane mbatizaji. “Watu wanasema, u Yohane Mbatizaji” Hoja ni kwamba Yohane alikuwa mtu mwenye msimamo siyo bendera fuata upepo. Alitoa sera zake bila kujali uso wa mtu. Askari walipomjia na kumwuliza wafanyeje, akawaambia waziwazi: “Msipokee rushwa, na msiwadhulumu watu.” Yohane Mbatizaji alikuwa mkweli hata kama ilimgharimu kukatwa kichwa.

Kwa hiyo, Yesu alilinganishwa na Yohane kwa sababu katika nafasi moja kabla ya kumwuliza juu ya haki ya kulipa kodi kwa Kaisari, walianza kwanza kumpa sifa kama za Yohane Mbatizaji: “Sisi tunajua kwamba wewe ni mtu wa haki, msema kweli, unafundisha njia za Mungu kwa ukweli, humpendelei yeyote na huangalii uso wa mtu yeyote.” Kwa hoja hiyo, watu walimhukumu Yesu kuwa anafanana na Yohane Mbatizaji.

Nabii mwingine anayelingana na Yesu ni Eliya. Huyu ni Nabii pekee anayeamini juu ya Mungu mmoja na analaani sana miungu wengi. Yesu analinganishwa na nabii Eliya katika kipengee hiki kwa sababu Yesu mwenyewe alisema yabidi kuchagua kimoja kwa sababu, “Huwezi kutumikia mabwana wawili.” Ukichagua kumfuata Mungu maisha yako yataongozwa kwenye uhuru, na ukweli. Ukifuata miungu wengine utakuwa mtumwa wa mali.

Kisha Yesu anafananishwa na Nabii Yeremia. Nabii huyu ndiye anayeonekana kushabihiana kwa karibu zaidi na Yesu. Nabii Yeremia alidhulumiwa vibaya sana na watu hasa na makuhani wa wakati wake kwa sababu alikuwa anapinga sana dini waliyokuwa wanaifuata iliyoonekana kuwa kama ya uganga wa kienyeji, yaani dini ya uwongo.

Katika kufuata dini hiyo walikuwa wanajitesa kwa mateso makali na kutolea sadaka ngumu ili kuinunua huruma ya Mungu. Wakashika taratibu ngumu za kufunga, za kufanya ibada mahekaluni kwa malengo ya kujipatia mibaraka toka kwa Mungu, ya kutaka mifugo yao izae zaidi, wapate mazao mengi, waweze kuepushwa na madhara ya nchi nk. Nabii Yeremia alizikosoa bila kuogopa ibada hizo kwa sababu zilikuwa ibada za kumnunua au kumlaghai Mungu.

Yesu analingana na roho hii ya Nabii Yeremia, kwa sababu aina hii ya mahusiano na Mungu hayana upendo ndani yake, bali ni mahusiano ya “nipe nikupe”. Kumbe Mungu hapigwi rushwa. Yesu alitaka mtu afuate roho ya sheria, na afanye mambo kwa haki, kwa heshima na kwa upendo.

Manabii waliokuwa wanahitajika ulimwenguni ni kama hawa waliokuwa wanahubiri haki na ukweli, waliokuwa wanamtetea Mungu mmoja na kumpa kipao mbele na kutompiga rushwa. Hivi ndivyo watu walivyokuwa wanamwona Yesu na sera zake.

Baada ya kujibiwa swali hili la jumla, katika swali la pili utaweza kumwona Yesu jinsi alivyokuwa mwana mapinduzi. Yaani, hakubaliani kabisa na kufuata dini kwa mtindo huo kwani kunakufanya ujione mkristu, kwa sababu tu umezaliwa katika mazingira ya ukristu au katika familia ya kikristu. Hatari ya dini namna hiyo inakufanya mtu kuwa mbishi, au kuwa mfuasi mkali wa dini na kuifuata kama siafu wanavyofuatana bila kujua wanakotoka wala wanakoenda.

Mapato mengine ni kwamba, imani hiyo inapotetereshwa na kutiwa majaribuni, mwamini unaanza kulinganisha imani yako na mila au utamaduni, na utaifa wako. Hapo ndipo unapokutana na mlokole (fanatic) au na mtu wa imani kali.

Kumbe, baada ya swali hilo la jumla Yesu anatoa swali la kuwajibisha. “Je ninyi mnanionaje?” Swali hili muhimu sana tungeweza kuliweka hivi: “mimi ni nani kwako au ninayo nafasi gani katika maisha yako?” Petro anajitosa kulijibu kwa niaba yetu. “Wewe ni Kristu (masiha), Mwana wa Mungu mzima.” Sehemu ya kwanza ya jibu la Petro laonekana amelikokotoa toka kwenye Katekisimu aliyofundishwa na marabi: “Wewe ni Kristu, ni Masiha, Mpakwa, Mshindi.”

Sehemu ya pili ya jibu ni “Wewe ni Mwana wa Mungu mzima.” Maana yake Yesu ni Emmanuel, Mungu nasi, ndiye sura au icon ya Mungu mzima. Kwamba, Mungu ni chemchemi ya uzima. Kwamba Yesu ameingia katika uzima, ameleta uzima zaidi. “Nimefika ili muwe na uzima tena muwe nao tele (Yoh. 10:10).

Yesu analikubali jibu hilo na anamwita Petro “Mwenye heri wewe yaani umebarikiwa”, kwa sababu siyo mwili uliokufumbulia hayo bali toka juu, kwa vile Petro hakujiacha kuongozwa na nia njema ya nafsi yake, au akili yake, bali kwa mwanga utokao kwa Mungu.Tukijiuliza sisi swali kama hilo, tukifaulu kulijibu sahihi, hapo ndipo tutajitosa kabisa kuishi maisha ya Yesu.

Toka hapa Yesu anatoa picha ya mwamba na ya funguo: Wewe Petro ni mwamba, na juu ya mwamba huo nitalijenga kanisa langu: na nitakupa wewe funguo za ufalme” Kwa hiyo Petro na waandamizi wake ni miamba, lakini kwa kigezo hiki kwamba wanaendelea kumshuhudia Yesu kuwa: “Wewe ni Mwana wa Mungu mzima”. Imani hiyo inamhusu kila mfuasi wa Kristu aliyemwona, aliyemgusa, aliyeshuhudia huyo Kristu.

Kisha Yesu anatoa mwito kwa wengine: “Msiwaambie watu wengine.” Hoja hii nayo inatutafakarisha, kwa sababu hata kama sisi tunaongea juu ya Kristu kuwa Yeye ni mkombozi, kuwa yeye ni mtoto wa Mungu, au tunasema Bwana asifiwe, lakini swali linabaki “umeelewa nini juu ya huyo Yesu unayemtamka. Umeugundua katika yeye uso wa Mungu ambao anauonesha? Swali linatuhusu sisi sote. Kwa hiyo kabla hujamweka Mungu kiti moto na kabla hujajitosa kumhubiri Yesu budi kujitia kiti moto wewe mwenyewe na kujihoji kama unamwelewa Yesu hasahasa na kama unaziishi kweli sera zake.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.