Ujumbe wa AMECEA kwa Familia ya Mungu na Watu wote wenye mapenzi mema
Mshikamano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati
AMECEA kwa watu wanaokabiliwa na majanga mbali mbali, umuhimu wa familia kama kiini
cha maisha ya kijamii, Uinjilishaji mpya na changamoto zake, umuhimu wa matumizi sahihi
ya teknolojia ya mawasiliano ya kisasa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, watoto
na vijana, wataalam wa Kikatoliki, seminari na nyumba za malezi, vitendo vya kigaidi
na uvunjifu wa misingi ya haki na amani, ni kati ya mambo makuu yaliyojitokeza katika
ujumbe wa AMECEA kwa Familia ya Mungu na kwa ajili ya watu wenye mapenzi mema katika
nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Mkutano mkuu wa 18 wa AMECEA uliokuwa unafanyika
mjini Lilongwe, Malawi umeongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji kwa njia ya wongofu
na ushuhuda wa imani ya Kikristo". AMECEA kwa namna ya pekee inamshukuru Baba Mtakatifu
Francisko kwa changamoto zake katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, mshikamano na
upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. AMECEA inaishukuru
Serikali ya Malawi kwa ukarimu na ushiriki wake mkamilifu katika maadhimisho ya mkutano
mkuu wa AMECEA. Wanawashukuru wadau mbali mbali waliojisadaka kwa ajili ya AMECEA.
AMECEA
inapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wananchi wote ambao wanakabiliwa na
hali ngumu ya maisha kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Ni matumaini
ya AMECEA kwamba, suluhu ya amani ya kudumu itapatikana katika maeneo ambayo bado
kuna vita na kinzani. Wananchi wanachangamotishwa kujikita katika misingi ya haki,
amani, upatanisho na umoja wa kitaifa.
AMECEA katika ujumbe wake inabainisha
kwamba, Familia ni kiini cha maisha ya kijamii, lakini kwa sasa inakabiliwa na matatizo
na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na: kuvunjika kwa misingi ya maadili na utu
wema, mashambulizi dhidi ya familia, umaskini na ukosefu wa fursa za ajira. AMECEA
kwa upande wake inasema, itaendelea kuzivalia njuga changamoto zote hizi ili kuimarisha
Familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Kanisa litaendelea kuzisaidia familia zilizovunjika
na zile ambazo kwa sasa zinakabiliwa na hali ngumu ya maisha na kwamba, inalaani unyanyasaji
unaofanywa majumbani.
AMECEA inapenda kukazia kuhusu umuhimu na udumifu wa
ndoa kati ya mwanaume na mwanamke kwa ajili ya kushiriki katika kuzaa na kulea watoto.
AMECEA inalaani harakati zozote zile zinazotaka kupindisha ukweli kuhusu taasisi ya
familia. Maisha ya kifamilia hayana budi kuheshimiwa, kulindwa na kudumishwa, ili
kujenga misingi ya haki, amani na utulivu.
Maaskofu wa AMECEA wanalaani ndoa
za watu wa jinsia moja, jambo linalokwenda kinyume cha ubinadamu na kanuni maadili.
Familia inapaswa kulindwa kwa gharama zote, ili kuiwezesha kuwa kweli ni chombo cha
Uinjilishaji mpya, ambao ni wa Kiafrika na Kikristo kweli! AMECEA inaendelea kuvuta
subira ili kupokea matunda ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya
familia.
AMECEA inasema, katika maadhimisho ya mkutano wake mkuu, imepembua
kwa kina na mapana changamoto na fursa za uinjilishaji mpya kwa kuangalia jinsi ambavyo
Wamissionari walivyotekeleza utume huu na kwamba, mihimili ya Uinjilishaji inahamasishwa
kuendelea kuwa ni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Katekesi makini, toba na wongofu
wa ndani, tasaufi ya kweli na ushuhuda thabiti ni mambo msingi kwa Wakristo ndani
na nje ya AMECEA. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ndogo
ndogo za Kikristo, kama sehemu muafaka za kushirikishana mang'amuzi ya imani.
Mababa
wa AMECEA wamekazia umuhimu wa matumizi sahihi ya teknolojia ya mawasiliano katika
mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Watoto na vijana walindwe na kufundwa
kikamilifu ili waweze kuwa ni vyombo vya haki na amani. Wanaziomba Serikali katika
nchi za AMECEa kuwekeza zaidi katika elimu na fursa za ajira ili kuwajengea vijana
uwezo wa kuishi kwa heshima. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwekeza katika majiundo
makini ya watoto na vijana.
Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa ni mahali pa kuwakutanisha watu mbali mbali na kwamba, kwa
njia ya elimu, Kanisa linaendelea kuwainjilisha watu na kuwajengea uwezo wa kuwajibika
barabara katika jamii zao. Wanafunzi katika taasisi hizi wapewe kanuni maadili na
maisha ya kiroho na kwamba, viongozi wa maisha ya kiroho watekeleze dhamana hii hata
nje ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu.
Wanataaluma Wakatoliki wataendelea
kufundwa katika imani, ili waweze kuwa kweli ni mashahidi amini na muhimu wanapotekeleza
dhamana yao Barani Afrika. Wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji
mpya. Seminari na nyumba za malezi ni sehemu muhimu sana za kufunda mihimili ya Uinjilishaji
na kwamba, hapa ni mahali pa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili kukidhi mahitaji kwa
kuendelea kusoma alama za nyakati. Walezi makini wanatakiwa Seminarini na kwenye nyumba
za malezi.
AMECEA inasikitika kusema kwamba, kwa miaka mingi nchi za AMECEA
zimekuwa zilifurahia amani na utulivu, lakini vitendo vya kigaidi na uvunjifu wa amani
vinaendelea kutishia usalama na maisha na wananchi wengi wa AMECEA. Wanaziomba Serikali
kuhakikisha kwamba, zinashirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kukomesha vitendo vya
kigaidi. Wanawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato
utakaosaidia kujenga na kudumisha uhuru wa kidini, uhuru wa dhamiri pamoja na kuheshimu
haki msingi za binadamu, kama msingi mkuu wa amani na utulivu.
AMECEA inapongeza
Serikali zile ambazo zimekuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu.
Inalaani mashambulizi yanayofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani,
changamoto kwa watu kuheshimiana na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene.
AMECEA inapenda kuungana na wote waliokumbwa na majanga mbali mbali wakati walipokuwa
wanaadhimisha mkutano mkuu wa kumi na nane huko Lilongwe, Malawi. Wanawatakia kheri
na baraka tele!
Ujumbe wa AMECEA kwa Familia ya Mungu na watu wenye mapenzi
mema, umetiwa sahihi kwa mara ya kwanza na Askofu mkuu Berhaneyesus Souraphiel, Mwenyekiti
mpya wa AMECEA.