Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa
Tunakuletea tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 18 ya mwaka A wa Kanisa. Unaalikwa
leo kushiriki furaha ya milele ambayo katika neno la leo inalinganishwa na sherehe
iliyo kubwa, nzuri na iliyosheheni vyakula vya aina zote. Kwa kushiriki sherehe hii
Nabii Isaya anasema hakuna malipo zaidi ya kuwa na mambo mawili yaani njaa na kiu.
Kwa jinsi
hii mimi mwenyewe lazima nitashiriki kwa maana nimepunguziwa gharama ya malipo isipokuwa
nadaiwa kupiga mwendo na kufika kwenye mazingira inapofanyika.
Hata hivyo tunapaswa
kujiuliza, hivi leo hii kuna sherehe katika miji, mitaa na vijiji vyetu isiyokuwa
na gharama? Kwa hakika naona ni kama hakuna! Kwa maana hiyo huyu anayetualika amepata
wapi fedha ya kufadhili sherehe nzima? Tena cha ajabu hakuna idadi kamili ya watu
inayohitajika, kwa jinsi hiyo sherehe hii inao uwezo wa kuwakirimu watu wote watakaofika.
Mpendwa
unayesafiri pamoja nasi leo, tunakualika sasa upate majibu ya maswali haya katika
injili. Tunamwona Mwana wa Mungu anayewalisha watu elfu tano wanaume pasipo kuhesabu
wanawake na watoto. Anawalisha kwa mikate mitano na samaki wawili! Hili ni jambo la
ajabu machoni petu, limefanywa na Mungu. Katika hali ya kawaida mikate mitano na visamaki
viwili visingeweza kutosheleza watu wote, kumbe kuna nguvu ya Mungu toka juu iliyojaa
upendo unaoshibisha wana wa Mungu.
Mpendwa msikilizaji, wanapokula wanasaza
na vikapu kumi na viwili vinakusanywa, ndiyo kusema kama Mungu akiwa katika maisha
yetu daima hatutatindikiwa na kitu chochote. Leo hii, zawadi hii tunapewa kwa njia
ya Ekaristi Takatifu mkate wa uzima wa mbinguni, usioisha wala kupungua kwa vizazi
vyote. Wajibu wetu si kupeleka pesa kununua bali kuwa na mapendo kwa wenzetu, imani
thabiti na maandalizi tafiti moyo yanayokagua uwepo wa neema ya utakaso mioyoni mwetu
na matamanio makamilifu mbele ya mkate huu wa uzima wa mbinguni. Matamanio yetu, imani
yetu na mapendo kwa wenzetu ndiyo njaa na kiu anayotuambia nabii Isaya.
Mtume
Paulo akiona utajiri wa Ekaristi Takatifu, utajiri usiodai gharama ya kifedha bali
gharama ya upendo, anaweka mbele yako swali lenye kugusa moyo wako na unapaswa kulijibu
kadiri ya mazingira yako. Je, kipi chaweza kututenga na upendo wa Kristu? Kipi chaweza
kututenga na Ekaristia? Mtume anatoa mwelekeo, je ni njaa, vishawishi? Hapana.
Natumai
wewe ni Baba, Mama, mtoto, mwanafunzi, afisa katika serkali, Kasisi. Je, yepi katika
mazingira yako yaonesha kukuvuta ili ujitenge na upendo wa Kristu? Yaone mapema na
uanze kujitenga nayo ili uunganike na Kristu aliyemwaga damu pale msalabani kwa ajili
yako.
Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwenu na Pd Richard Tiganya
C.PP.S.