2014-07-31 12:20:43

Ratiba elekezi ya Papa Francisko nchini Albania!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Septemba 2014 anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Albania. Ratiba iliyotolewa na Vatican inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma majira ya saa 1: 30 asubuhi na kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mama Theresa wa Calcutta saa 3: 00 ambako atapokelewa na Waziri mkuu wa Albania Bwana Edi Rama. Saa 3: 30 Baba Mtakatifu atapata mapokezi ya kitaifa na baadaye atafanya mazungumzo ya faragha na Rais wa Albania.

Ratiba inaonesha kwamba, saa 4:00 asubuhi, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, kwenye Ikulu ya Albania. Saa 5:00 ataadhimisha Ibada ya Misa takatifu na baadaye kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na waamini kwenye Uwanja wa Mama Theresa wa Calcutta. Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko atakutana na baadaye atapata chakula cha mchana na Maaskofu Katoliki wa Albania.

Saa 10:00 jioni, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa dini mbali mbali nchini Albania. Saa 11:00 atasali masifu ya jioni na Mapadre, Watawa, Waseminaristi na Vyama vya Waamini walei, tukio ambalo litafanyika kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu Tirana.

Baadaye saa 12:30 jioni, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na watoto pamoja na watu wanaojitolea kwenye Kituo cha Betania. Saa 1:45, Baba Mtakatifu Francisko ataagana na wenyeji wake na hatimaye kufunga vilago kuanza safari ya kurejea tena mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.