Papa ni mjumbe wa upendo na huruma, ameguswa na mahangaiko ya watu!
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini katika barua yake ya kichungaji iliyochapishwa
hivi karibuni baada ya kuhitimisha mkutano wake wa 109 wa mwaka linasema kwamba, hija
ya kitume inayotarajiwa kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko nchini humo mwanzoni
mwa mwezi, yaani kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 19 Januari 2015 ni kutaka kuwashirikisha
wananchi wa Ufilippini ujumbe wa kichungaji unaojikita katika misingi ya upendo, huruma
na kuguswa na mahangaiko ya watu.
Baba Mtakatifu
Francisko atakuwa ni Papa wa tatu kutembelea Ufilippini baada ya watangulizi wake
Paulo V Ina Mtakatifu Yohane Paulo II. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko
inalenga kuwaimarisha ndugu zake katika imani kwa Kristo na Kanisa lake, ili waweze
kuwa tayari kutolea ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo sanjari na kukabiliana
na changamoto mbali mbali za maisha, pasi na kukata wala kujikatia tamaa. Ni mwaliko
wa kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuwatangazia wengine Injili ya Furaha.
Maaskofu
wanasema, Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wananchi wote wa Ufilippini kusonga
mbele kwa imani na matumaini baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha
majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Waamini na wananchi wa Ufilippini
katika ujumla wao wanaalikwa kuanzia sasa kujiandaa kwa makini kukutana na Baba Mtakatifu
Francisko, kwa kujivika mioyoni mwao fadhila ya unyenyekevu na huruma zinazopaswa
kumwilishwa kila siku ya maisha yao.
Maaskofu wanasema, fadhila hizi zinaweza
kutekelezwa kwa kuwafundisha watoto Biblia, kuwasaidia jirani zao wanaohitaji msaada
wa hali na mali; kwa kuwatembelea na kuwasaidia wagonjwa na wafungwa. Lakini jambo
la msingi katika maisha ya kiroho ni kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kuziishi
Sakramenti za Kanisa kwa kujiandaa vyema. Kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ekaristi
Takatifu iwasaidie waamini kupata nguvu ya maisha ya kiroho inayobubujika kutoka kwa
Kristo mwenyewe, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa
na Jamii kwa ujumla.
Waamini waonje huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya
Sakramenti ya Upatanisho pamoja na kuzisaidia Familia zao kuwa kweli ni shule ya sala
na utakatifu wa maisha; Familia Kanisa dogo la nyumbani, linalosali, linalotafakari
Neno la Mungu na kulimwilisha katika imani tendaji. Yote hii ni mikakati inayoweza
kuwasaidia waamini pamoja na wananchi wa Ufilippini kujiandaa kwa ajili ya ujio wa
Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao.
Katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa
Baraza la Maaskofu wa Ufilippini, wamekazia umuhimu wa wananchi kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa kitaifa, kama kielelezo cha furaha yao kwani wote wameumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu. Changamoto hii wanasema Maaskofu Katoliki wa Ufilippini
inapaswa kujionesha katika ngazi mbali mbali ya maisha, kwa kushuhudia ule wito wa
kuwa kweli ni watoto wa Mungu. Wasimame kidete kulinda na kutetea Injili ya maisha
pamoja na kuendelea kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya nchi
yao, huku utu na heshima ya mwanadamu ikipewa kipaumbele cha kwanza.
Maaskofu
wanasema changamoto hii iguse dhamiri za wanasiasa, ili waweze kubadili na kuanza
mchakato utakaosaidia kutibu na kung’oa kabisa Saratani ya rushwa, ufisadi na wizi
wa mali ya umma, janga ambalo kwa sasa ni la kitaifa. Wanasiasa wanapaswa kujipambanua
kwa kuonesha kwamba, uongozi ni huduma inayopania kusimamia na kutekeleza mafao ya
wengi, utu na heshima ya binadamu.
Maaskofu wanawataka Makleri kuonesha ile
sura ya Kristo mchungaji mwema anayejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Wanakondoo
wake. Katika historia ya maisha ya Kanisa nchini Ufilippini, kuna baadhi ya Makleri
wameelemewa mno na ubinadamu kiasi cha kusababisha kashfa na makwazo kwa Familia ya
Mungu. Lakini bado kuna kundi kubwa la Makleri na Watawa wanaoendelea kujisadaka kwa
ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii bila upendeleo.
Ni
wajibu wa wananchi wote wa Ufilippini kulinda na kutunza mazingira kama sehemu ya
urithi wa kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu kwa ajili
yake na kwa ajili ya kizazi kijacho. Uchafuzi wa mazingira na ukataji ovyo wa misitu
ni mambo ambayo ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya watu. Ni wajibu wa kila mtu kulinda
na kutunza mazingira; kujenga na kuendeleza moyo wa mshikamano, kwa kusaidiana na
kuwajibikiana kama ndugu wamoja wanaopania kukuza fadhila ya uaminifu inayojikita
katika ushuhuda wa maisha. Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.