Baba Mtakatifu Francisko anasubiriwa nchini Korea kama mjumbe wa amani na wananchi
wa Korea ambao kwa takribani miaka hamsini wameendelea kuteseka kutokana na kinzani
na mgawanyiko, changamoto ya kuanza mchakato wa kuponya madonda ya utengano kati ya
Korea hizi mbili, tayari kujikita katika mchakato wa uponyaji na upatanisho.
Ni matumaini
yanayooneshwa na Professa Thomas Hong-soon Han wa masuala ya siasa za uchumi kutoka
Chuo Kikuu cha Hankuk, ambaye amewahi pia kuwa Balozi wa Korea mjini Vatican, katika
mahojiano maalum na Jarida la “La Gregoriana” linalochapishwa na Chuo Kikuu cha Kipapa
cha Gregoriani, kilichoko mjini Roma.
Profesa Thomas anasema, wananchi wa
Bara la Asia wanamsubiri kwa hamu kubwa Baba Mtakatifu Francisko, ili kushirikishana
ile Furaha ya Injili. Kutokana na ushawishi wake mkubwa katika masuala ya Mafundisho
Jamii ya Kanisa, Professa Thomas alifaulu kuanzisha Chuo cha Mfundisho Jamii ya Kanisa
nchini Korea, chuo ambacho kinachngia kwa kina katika demokrasia na maendeleo ya wananchi
wote wa Korea.
Anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mchango mkubwa unaotolewa
na Mama Kanisa kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu pamoja
na maendeleo endelevu ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Bara la Asia lina kiu ya haki
na amani, upendo na mshikamano wa kweli. Katika miaka ya hivi karibuni, Bara la Asia
limeendelea kucharuka katika uchumi na maendeleo ya vitu, lakini limeendelea kutopea
katika uvunjaji wa haki msingi za binadamu.
Ni sehemu ambayo ina kinzani kubwa
za kidini kutokana na baadhi ya waamini kuwa na misimamo mikali ya kidini ambayo haina
tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu husika. Bara la Asia linakabiliwa
na uchafuzi mkubwa sana wa mazingira, hali inayopelekea pia uwepo mkubwa wa maskini
na watu wanaoshambuliwa na magonjwa.
Professa Thomas anasema, Mafundisho Jamii
ya Kanisa yanawasaidia waamini na wananchi katika ujumla wao kutolea ushuhuda wa tunu
msingi za maisha ya mwanadamu na kwamba, Imani kwa Kristo na Kanisa lake si jambo
linalotishia ustawi na maendeleo ya wananchi wa Bara la Asia, bali ni kikolezo kikuu
cha utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi.
Korea na Vatican,
Desemba 2013 wameadhimisha Jubiulee ya Miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya
pande hizi mbili. Katika kipindi chote hiki, Vatican imeendelea kushirikiana na Korea
katika medani mbali mbali za maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wanachi wa
Korea. Kazi kubwa kwa sasa ni kusaidia utekelezaji wa mchakato wa upatanisho kati
ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini, ili wote waweze kujisikia kuwa ni watu wa
taifa moja