2014-07-31 08:56:36

Kanisa linataka kuwasilikiza wanafamilia kwa moyo wote!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anabainisha kwamba, Mama Kanisa anapoendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha ya ndoa na familia anapenda kwa namna ya pekee kujikita katika hija ya kusikiliza Neno la Mungu pamoja mahangaiko ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. RealAudioMP3

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki, watu wamepewa fursa ya kutoa maoni yao ili kujenga utamaduni wa mantiki ya Kanisa kusikiliza kwa makini na hatimaye kutenda kwa ujasiri. Kanisa kama Jumuiya ya waamini kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema ili kutafuta majibu muafaka ya changamoto zinazoendelea kumkabili mwanadamu katika maisha ya ndoa na familia limeamua kufanya maadhimisho ya Sinodi, kipindi cha kusali, kutafakari na kutenda. Watu wana matatizo, wanazo changamoto za maisha, wana machungu na wasi wasi, lakini pia wana matumaini na furaha wanayosali na kuwashirikisha wengine.

Kardinali Baldiselli anasema, mantiki hii imeliwezesha Kanisa kupambanua tema itakayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014. “Changamoto za kifamilia mintarafu Uinjilishaji mpya” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya, ambayo yamepata baraka ya pekee kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayelihamasisha Kanisa kusikiliza kwa moyo, huruma na upendo wa kibaba.

Sinodi ya maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakuwa ni hija ya Familia ya Mungu kutembea kwa pamoja. Tayari kazi ya kukusanya na kuhariri majibu yaliyokusanywa na kuhaririwa na Mabaraza ya Maaskofu mahalia imekamilika na hapo tayari kuna Hati ya kutendea Kazi ijulikanayo kwa lugha ya Kilatini, Instrumentum Laboris.

Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, maadhimisho ya Sinodi yatakuwa katika awamu kuu mbili: Awamu ya kwanza itakuwa ni kusikiliza na kupokea ushuhuda kutoka kwa watu mbali mbali, ili kuishi na kutangaza kwa ari na moyo mkuu Injili ya Familia. Awamu ya Pili ya Maadhimisho ya Sinodi hii yatafanyika kunako mwaka 2015 ili kubainisha mwongozo wa jumla utakaotumika katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya binadamu na familia kwa ujumla.

Awamu zote mbili ni mwendelezo wa maadhimisho ya tukio hili kubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji mpya, changamoto inayovaliwa njuga kwa sasa na Mama Kanisa mintarafu mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa ambalo ni mwanga wa mataifa, linatumwa kutangaza furaha na matumaini kwa kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha Injili ya Furaha katika maisha yao.

Katika maadhimisho haya kutakuwa na hati tatu zitakazotolewa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Jamii ya mwanadamu kwa sasa inahitaji kuangaliwa kwa jicho makini zaidi, ili kubainisha changamoto za kichungaji na hatimaye, kuzifanyia kazi. Kati ya changamoto hizi ni ndoa mchanganyiko zinazofungwa kati ya Wakatoliki na waamini wa dini nyingine; familia ya mzazi mmoja, ndoa za wake wengi, mila na tamaduni zilizopitwa na wakati; myumbo wa familia kiasi cha kusambaratika hata katika uchanga wake; kuyumba kwa mahusiano ya ndoa na matokeo yake ni watu kukimbilia katika “nyumba ndogo” au kwenda “mchepuko” kama wanavyosema waswahili.

Katika maisha ya ndoa na familia bado mfumo dume unatawala sehemu nyingi za dunia na kuna baadhi ya nchi wanawake wanashika usukani. Wahamiaji na changamoto za maisha ya ndoa na familia; dhana ya familia na madai ya ndoa za jinsia moja na dhamana ya malezi kwa watoto wanaoasiwa ni kati ya matatizo yanayoikabili familia ya mwanadamu.

Vyombo vya mawasiliano ya jamii: uzuri na madhara yake katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Tatizo la uzazi wa chupa, tafsiri mpya kuhusu haki msingi za binadamu na sheria zake; ukanimungu na Sakramenti ya ndoa na Upatanisho kutopewa umuhimu unaostahili. Yote haya ni mambo ambayo yamejadiliwa kwa kina na mapana katika Hati ya Kutendea Kazi, Instrumentum Laboris.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, hii ni kazi ya nguvu iiyofanyika kuanzia mwaka 2013 inagusa kwa namna ya pekee mada kuhusu maisha ya ndoa na familia. Kwa mara ya kwanza waamini na watu wenye mapenzi mema wameshiriki kwa wingi kuchangia katika maswali dodoso yaliyotolewa. Maadhimisho ya Sinodi yatawashirikisha Watu wa Mungu, ili kuonesha umoja na mshikamano katika tofauti inayojikita katika karama, mapaji, utume na ufahamu wa mambo.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.