2014-07-30 09:56:41

Sitisheni biashara ya silaha kwa Syria, ili kukomesha vita!


Shirika la kutetea amani kimataifa, Pax Christi, linauomba Umoja wa Mataifa kupiga rufuku biashara ya silaha nchini Syria na kuanzisha tena mchakato wa majadiliano yanalenga kutafuta amani kwa kuzihusisha pande zote zinazohusika katika mgogoro huu.

Huu ndio mkakati pekee utakaoiwezesha Syria kusitisha vita na amani kuanza kutawale tena, chini ya udhibiti wa Umoja wa Mataifa. Katika vita hii, kuna mataifa ambayo yanaendelea kufanya biashara ya silaha na Syria, kiasi kwamba, maafa yanazidi kuongezeka siku hadi siku.

Pax Christi linasema, licha ya Jumuiya ya Ulaya kupiga rufuku biashara ya silaha na Syria, lakini Syria imeendelea kununua silaha na kwamba, jitihada za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2011 halijafanikiwa kupata suluhu ya kisiasa kuhusiana na vita huko Syria. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu laki moja na sitini wamekwishafariki dunia na wengine laki sita hawana makazi maalum na kwamba, nusu ya wananchi wa Syria wamegeuka kuwa wakimbizi hata katika nchi yao wenyewe.

Pax Christi inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha kabisa biashara ya silaha nchini Syria na kuanzisha mara moja mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa. Pax Christi inaupongeza Umoja wa Mataifa kwa kumteuwa Bwana Staffan de Mistura kuwa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria. Ulinzi na usalama kwa wananchi wa Syria ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Watu wanaokimbia vita na dhuluma waoneshwe ukarimu na Jumuiya ya Kimataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.