2014-07-30 08:57:10

Sifa za Askofu!


Bila shaka waamini na watu wenye mapenzi mema wanajiuliza maswali ambayo wakati mwingine wanashindwa kuyapatia majibu ya mkato! Inakuaje, Jimbo Katoliki linakuwa wazi kwa miaka kadhaa bila ya kupata Askofu wake ambaye, kimsingi ndiye mchungaji mkuu? RealAudioMP3

Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu anabainisha kwamba: Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa sala, kiongozi anayejipambanua kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake adili na matakatifu.

Ni kiongozi anayepaswa kuwa kweli ni mchungaji mwema, anayetambulikana pia kutokana na harufu ya kondoo wake, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Kimsingi haya ndiyo mambo msingi ambayo yanapaswa kuoneshwa na Askofu au wale wanaotamani kufikia utimilifu wa Daraja Takatifu la Upadre ambalo kimsingi limegawanyika katika madaraja makuu matatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi, kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Haya si mambo mapya anabainisha Kardinali Marc Ouellet, kwani Askofu anapaswa kuwa ni shahidi aminifu wa Kristo na Kanisa lake; mtu wa sala na tafakari ya Neno la Mungu; kiongozi ambaye ataonesha kwa maneno na maisha yake kwamba, uongozi kwake ni huduma na wala si cheo! Kwa wanajimbo wake anapaswa kuwa kweli ni mfano wa Baba na Kaka; mpole na mnyenyekevu wa moyo, mwingi wa huruma na mapendo; mvumilivu na mwenye hekima.

Baba mwema anayejitaabisha kuwachanga kondoo wake, kwa kuwaonesha dira na mwelekeo wa maisha; daima akikazia umoja, upendo na mshikamano, ili kati ya Kondoo wake, asiwepo anayepotea njia, Askofu awe kweli ni kiongozi anayekesha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, pasi na kumezwa na malimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anataka kuona Kanisa ambalo halina makuu, Kanisa linalojitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hawa ni maskini wa kiroho, hali na kipato. Kanisa ambalo uwezo na nguvu yake haitokani na mali au utajiri wake, bali neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hili ni Kanisa linalopaswa kuiga na kufuata mfano wa Yesu aliyekuwa: fukara, mtii na mseja kamili. Kanisa halina budi anasema Kardinali Marc Ouellet kuendeleza utume wa Yesu kwa kuwatangazia watu Injili ya Furaha. Kanisa liwasaidie watu kukutana ili hatimaye, liweze kuambatana na Yesu katika maisha yao.

Kumbe, Kanisa linachukua muda kupima na kuangalia ili kupata kiongozi atakayeunganisha familia ya Mungu, ili iweze kuwa kitu kimoja na chini ya mchungaji mmoja ambaye kimsingi ni Yesu Kristo mwenyewe! Awe ni kiongozi mwenye mwono mpana anayeweza kukabiliana na changamoto za kichungaji akiwa na “kifua kipana”.

Awe ni kiongozi anachota utajiri wa maisha na utume kwa ajili ya Familia ya Mungu katika chemchemi ya:Maandiko Matakatifu, Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Sakramenti za Kanisa, Jumuiya ya waamini na marafiki wa Yesu waliojipambanua kwa maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Kwa maneno mengine hawa ni kama vile Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, Mitume, Watakatifu na wafiadini; watu waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Askofu awe ni kiongozi mwenye ari na mwamko wa kimissionari anayetaka kuhakikisha kwamba, watu wanaendelea kutangaziwa Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha. Waamini wajisikie kuwa ni sehemu kubwa ya Familia ya Mungu inayowajibika.

Kardinali Marc Ouellet anasema, umoja, upendo na mshikamano kati ya Maaskofu ni jambo la msingi na hili linakaziwa sana na Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu. Hapa ni mahali pa kusali, kutafakari na kushirikisha uzoefu, mang’amuzi na vipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa. Papa Francisko ni kiongozi anayependa kusikiliza ushauri na mawazo kutoka kwa ndugu zake katika Kristo ndiyo maana ameunda Baraza la Makardinali linalomsaidia katika kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hili ni Baraza linaloundwa na Makardinali tisa, C9!

Mshikamano unaoneshwa kwa njia ya upendo na kwa kuguswa na mahitaji ya Makanisa mengine, sehemu mbali mbali za dunia. Mshikamano wa upendo unaweza kujionesha kwa njia ya rasilimali watu, fedha na vitu. Leo hii haishangazi kuona kwamba, kuna Mapadre kutoka Afrika na Amerika ya Kusini wakiwahudumia waamini katika nchi za Ulaya, ambazo kweli zilikuwa ni chimbuko la Ukristo na kazi za kimissionari kwa Bara la Afrika na Asia, lakini leo hii mambo yamebadilika, kumbe kunakutegemeana na kusaidiana katika kutangaza Injili ya Furaha kwa Watu wa Mataifa.

Mshikamano huu unapaswa kujionesha pia kwa njia ya Mabaraza ya Maaskofu katoliki katika nchi husika na katika kanda mbali mbali ndani ya Kanisa, ili kutafuta suluhu ya matatizo, fursa na changamoto zinazowatatiza waamini katika Makanisa Mahalia. Khalifa wa Mtakatifu Petro anaonesha mshikamano na Maaskofu wakati wa hija zao za kitume zinazofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Huu unakuwa ni wakati wa kusali, kuzungumza na kushirikishana na Baba Mtakatifu maisha na utume wa Makanisa mahalia. Hapa Maaskofu wanakutana pia na wakuu wa Mashirika ya Kipapa.

Kardinali Marc Ouellet anasema, Kanisa linaendelea kuutafakari Waraka wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa, kwa kuzingatia karama za mashirika ya kitawa na kazi za kitume; kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kumbe hapa kuna haja kwa Maaskofu kushirikiana na kushikamana na Watawa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu linaendelea kuwaalika Maaskofu kufanya toba, mageuzi na wongofu wa ndani kwa kujikita katika maisha ya kiroho zaidi. Wajitahidi kujipatia muda wa kusali na kutafakari, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Baraza litaendelea pia kuwasaidia Maaskofu katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.