2014-07-30 12:13:11

Marehemu Kardinali Marchisano alikuwa ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya elimu na utamaduni


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 30 Julai 2014 ameongoza Ibada ya mazishi ya Kardinali Francesco Marchisano. Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ndiye aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Kardinali Marchisano, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Katika mahubiri yake amemkumbuka Marehemu ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 85, miaka 62 ya huduma kwa Mungu na Kanisa na miaka 58 kwa ajili ya utume ndani ya Vatican.

Kardinali Marchisano ni mtu aliyekuwa anatekeleza dhamana na utume wake katika hali ya ukimya. Aliyaangalia mahitaji ya maskini na hasa viziwi, utume alioufanya kwa miaka thelathini. Alijielekeza zaidi katika masuala ya elimu katoliki, utamaduni na urithi wa Kanisa. Aliteuliwa kuwa Kardinali na Mtakatifu Yohane Paulo II na baadaye akatekeleza dhamana yake kama kiongozi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Kardinali Marchisano, anasema Kardinali Sodano kwamba, ni utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwa kumpumzisha mja wake katika usingizi wa milele, lakini zaidi kwa kazi ya uumbaji, ukombozi na matendo makuu anayofanya kwa ajili ya Kanisa lake. Ibada hii pia ni kwa jili ya kuomba msamaha na huruma ya Mungu kutokana na dhambi za waja wake, hata kama Kanisa ni takatifu, lakini daima linahitaji kusafishwa.

Waamini wanaalikwa kuliangalia Fumbo la Kifo kwa kumtazama Yesu na kwamba, siku moja ataigeuza miili yao ili ifanane na Mwili wake Mtakatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.