Serikali ya Chad inaridhishwa na mahusiano kati yake na Vatican
Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini Chad, hivi karibuni aliwasili
nchini Chad na kupokelewa na viongozi wa Kanisa mahalia, tayari kuanza utume wake
nchini humo kwa kuwasilisha hati za utambulisho kwanza kabisa kwa Waziri wa mambo
ya nchi za nje na ushirikishano wa kimataifa Bwana Moussa Mahamat Dabo.
Serikali
ya Chad inaridhika na uhusiano mwema uliopo kati yake na Vatican na kwamba, inatambua
mchango mkubwa unaotekelezwa na Kanisa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.
Askofu
mkuu Coppola akiwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais Idriss Dèby Itno wa Chad
aliyekuwa ameambatana na viongozi mbali mbali wa Serikali, Rais amemshukuru kwa namna
ya pekee baba Mtakatifu Francisko kwa maisha na utume wake kwa ajili ya Kanisa, lakini
zaidi kama mtetezi wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Serikali
ya Chad itaendelea kuunga mkono juhudi za Kanisa mahalia katika kumhudumia mtu mzima:
kiroho na kimwili.
Kanisa Katoliki linapenda kukuza na kuendeleza majadiliano
ya kidini na kiekumene, ili kujenga misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa
kitaifa, watu wakiheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao
za kidini, kikabila na mahali anapotoka mtu! Kanisa litaendeleza mchakato wa kudumisha
amani kwa kuwashirikisha vijana ambao kimsingi ndio wadau wakuu wanaoweza kujenga
au kubomoa amani, ikiwa kama hawatafundwa kikamilifu.
Chad imeendelea kuwa
ni mfano bora wa kuigwa Barani Afrika kwa wananchi wake licha ya tofauti zao za kidini
kuendelea kuheshiminiana na kuishi pamoja kama watoto wa Baba mmoja.
Askofu
mkuu kama sehemu ya utambulisho wake, ameadhimisha pia Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa
na Familia ya Mungu nchini Chad. Ametumia fursa hii kuwasilisha hati zake za utambulisho
kutoka kwa Katibu mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin na kumkabidhi Askofu Jean
Claude Bouchard, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Chad.