Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, tarehe 27
Julai 2014 limeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 45 tangu SECAM ilipoanzishwa kwa mara
ya kwanza wakati Mtumishi wa Mungu Paulo VI alipotembelea Uganda kunako mwaka 1969.
Hili lilikuwa ni tukio la kihistoria kwani ni kwa mara ya kwanza kabisa Khalifa wa
Mtakatifu Petro alikuwa anatembelea Bara la Afrika.
Leo hii SECAM inaundwa
na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kitaifa yapatayo 37 yanayowakilishwa na Mashirikisho
ya Mabaraza ya Maaskofu Kikanda yapatayo 8, kati yake ni AMECEA, lililohitimisha mkutano
wake wa kumi na nane uliokuwa unafanyika mjini Lilongwe, nchini Malawi.
Kwa
mara ya kwanza katika historia, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
na Madagascar, SECAM, limeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 45 tangu kuanzishwa kwake,
kwa kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa la Kiulimwengu, lakini zaidi kwa ajili ya
maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. SECAM pamoja na mambo mengine inapania kuwa
na mwono wa pamoja kuhusu Kanisa Barani Afrika, dhana ambayo imekuwa na kukomaa kutokana
na changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Bara
la Afrika linatambua utajiri mkubwa unaofumbatwa katika lugha, mila, desturi na tamaduni
mbali mbali zinazopatikana Barani Afrika, lakini hata hivyo bado linahamasishwa kujenga
na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa Barani Afrika, ili kwa pamoja Familia ya
Mungu inayowajibika Barani Afrika iweze kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya
unaojikita katika utamadunisho, upatanisho, haki na amani, mambo ambayo Kanisa Barani
Afrika linapenda kuyavalia njuga kama sehemu ya mikakati yake ya Uinjilishaji wa kina
unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Kanisa Barani Afrika linatambua
umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli amani na maendeleo
ya watu yaweze kupatikana. Kanisa Barani Afrika litaendelea kujielekeza zaidi na zaidi
katika Uinjilishaji wa awali kwani bado kuna umati mkubwa wa watu ambao bado haujabahatika
kusikiliza Injili ya Furaha.
Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa njia ya
ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, ili kweli Ukristo uweze kuwa na mashiko
na mvuto kwa watu wa nyakati hizi sanjari na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa
na familia na kwamba Bara la Afrika si dodoki linalokusanya kila aina ya takataka
zinazotolewa na vyombo vya habari. Bara la Afrika lina mila, tamaduni na maadili yake
yanayopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani
Afrika.
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.