2014-07-26 09:40:16

Makanisa yanahimizwa kushirikisha mawazo katika mchakato wa maendeleo endelevu!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kuyahimiza Makanisa ya Kikristo kushiriki kikamilifu katika majadiliano yaliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa, ili kubainisha na kuweka mikakati ya maendeleo baada ya kuhitimisha Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kuyahimiza Makanisa kushiriki katika majadiliano haya, ili kubainisha vipaumbele vinavyopaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya mwanadamu.

Mambo yafuatayo yanaendelea bado kupewa uzito wa pekee na Jumuiya ya Kimataifa: mikakati ya kupambana na baa la umaskini duniani, usawa wa kijinsia, mikakati ya kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi ili kushiriki kikamilifu katika mikakati ya kujikwamua kiuchumi na kijamii. Jumuiya ya Kimataifa inaangalia uwezekano wa kuwa na mipango endelevu kuhusu mipango miji, utunzaji bora wa mazingira na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi bila kusahau umuhimu wa Jumuiya ya watu kujikita katika mchakato wa upatanisho.

Yote haya ni mambo ambayo waamini wa Makanisa mbali mbali wanaweza kuchangia ili hatimaye, kupata muafaka wa mikakati ya maendeleo itakayovaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa mara baada ya mwaka 2015. Makanisa yanaweza kushirikisha mchango wao kwa njia ya Nyaraka, mawazo na upembuzi yakinifu na kuwasilisha kwenye Umoja wa Mataifa kabla ya tarehe 8 Agosti 2014. Mawazo ya majadiliano haya yatausaidia Umoja wa Mataifa kuandaa taarifa itakayofanyiwa kazi baadaye!

Itakumbukwa kwamba, tangu Mwaka 2000 Jumuiya ya Kimataifa ilijiwekea Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Miaka yote hii imetumiwa na Jumuiya ya Kimataifa kujadili kwa kina na mapana mikakati ya maendeleo endelevu kwa ajili ya Jumuiya ya Mwanadamu. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, lengo la majadiliano kwa njia ya mitandao ya kijamii ni kutaka kuwashirikisha watu wengi zaidi katika kuibua mawazo, uzoefu na vipaumbele ambavyo vinapaswa kufanyiwa kazi na Umoja wa Mataifa kwa miaka ijayo.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Makanisa yamekuwa ni wadau wakuu wa maendeleo ya mwanadamu hasa katika sekta ya elimu na afya. Makanisa yakishirikishwa kikamilifu yanaweza kuchangia mwelekeo mpya wa maendeleo ya mwanadamu!







All the contents on this site are copyrighted ©.