Utu na utakatifu wa maisha ya binadamu ni mambo nyeti!
Kardinali Timothy Michael Dolan wa Jimbo kuu la New York, Marekani katika tafakari
yake kuhusu mateso na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi nchini Marekani anasema
kwamba, kuna haja ya Jamii kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.
Hivi karibuni ameshuhudia umati mkubwa wa wananchi waliokuwa na hasira wamezunguka
Bus lililokuwa limewabeba wahamiaji, wakimbizi na omba omba wa mjini Calfornia, wakipiga
kelele kutaka waondolewe mara moja kutoka mjini humo!
Jambo hili limemfadhaisha
sana Kardinali Dolan kwani ni kitendo ambacho ni kinyume kabisa cha utu na heshima
ya binadamu; ni kitendo kinachosigana na Maandiko Matakatifu. Wananchi waliokuwa na
hasira walifanikiwa kwani Madreva waliokuwa wanaendesha Mabus hayo, waliogopa na kutafuta
hifadhi sehemu nyingine. Kwa watu wenye umri mkubwa wanakumbuka unyama kama huu waliotendewa
wahamiaji na wageni waliokuwa wanatafuta hifadhi nchini Marekani.
Wananchi
wengi wa Marekani wanasahau kwamba, wengi wao ni wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali
za dunia, waliofika nchini humo wakiwa wamegubikwa na baa la njaa na umaskini, lakini
wakiwa na tumaini la maisha bora zaidi.
Mjini Texas, Marekani hali ni tofauti
kabisa, wananchi wanaonesha upendo na ukarimu kwa wahamiaji na wageni waliofika kwenye
Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Wafanyakazi wa Serikali walitekeleza wajibu wao
kwa utaratibu pasi na makelele, jambo ambalo anasema Kardinali Dolan, limemfurahisha
na kumpatia faraja. Hapa inaonesha umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea utu,
heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu. Ni jambo la fedhehesha sana kuwashambulia
watu wenye shida wanaohitaji kuonjeshwa huruma na upendo!