2014-07-25 11:01:56

Kampeni dhidi ya biashara haramu ya binadamu!


Umaskini wa kipato na hali pamoja na kuporomoka kwa misingi ya maisha ya ndoa na familia ni kati ya sababu kubwa zinazoendelea kuchangia kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ni kati ya mambo ambayo yamewapelekea hata baadhi ya wazazi, ndugu na jamaa kuwatoa watoto wao kafara katika biashara haramu ya binadamu inayoendelea kushamiri sehemu mbali mbali za dunia.

Ukosefu wa elimu bora, majanga asilia, kinzani na myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya mambo yanayoendelea kuwatumbukiza watoto, wasichana na wanawake kwenye biashara haramu ya binadamu Barani Afrika na Asia. Biashara haramu ya binadamu ni mtaji mkubwa kwa watu wanaojihusisha na biashara hii ambayo kimsingi iko kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Kutokana na kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu, Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco nchini Benin limeanzisha kampeni maalum kwa ajili ya kuwalinda watoto wasitumbukizwe kwenye biashara haramu ya binadamu. Biashara hii inadhalilisha utu na heshima ya binadamu na kuwapoka watoto matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hali inatisha nchini Benin pengine na hata katika nchi kadhaa Barani Afrika.

Wazazi kutokana na umaskini na uchu wa fedha wanaamua kuwasaliti hata watoto wao wenyewe, hali inayoonesha kufilisika kwa watu kimaadili na kiutu. Inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya watoto millioni moja ambao ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu kadiri ya takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Kazi Duniani, ILO. Kisingizio cha kutaka kuwaasi watoto kinyume cha sheria, ndoa za shuruti pamoja na biashara haramu ya viungo vya binadamu ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuchochea kasi ya biashara haramu ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.