2014-07-24 15:52:58

Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu, Mombasa, Kenya waanza mkutano wao mkuu!


Utawa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Watu wa Mungu na kwamba, maisha ya kitawa ni kiungo kikuu katika maisha na utume wa Kanisa, katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, unaopania kueneza Ufalme wa Mungu unaojikita katika haki, amani, upendo na mshikamano. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Padre Willybard Lagho, Makamu Askofu, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya.

Mkutano huu unaadhimishwa kwenye nyumba asili ya Masista hawa iliyoko Bura, Taita, Jimbo kuu la Mombasa na umefunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza katika maisha na utume wao, hususan kipindi hiki wanapofanya mapitio katika maisha na utume wao kwa Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Maamuzi yatakayofanywa na wajumbe wa mkutano huu yatakuwa na mwangwi si tu kwa watawa wenyewe bali kwa Kanisa na Jamii, kwani wanasukumwa kuangalia maisha na utume wao kwa kuzingatia: Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya Kanisa, Kanuni za Shirika na Sheria za Kanisa, kwani mambo haya ni nguzo na msingi wa maisha na utume wa Masista wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya.

Akiwakaribisha wajumbe kushiriki katika maadhimisho ya mkutano huu, Sr. Ursula Lyimo, Mama Mkuu wa Shirika amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka alizoweza kulikirimia Shirika katika kipindi cha miaka sita, ya uongozi wake. Amewataka watawa wake kushiriki kwa uaminifu na ukamilifu, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili apate kuwaongoza na kuwasindikiza katika maadhimisho ya mkutano mkuu.

Mkutano huu utahitimishwa kwa uchaguzi wa viongozi wakuu wa Shirika kwa kipindi kingine cha miaka sita. Kanisa linaungana na Watawa hawa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maisha na utume wa watawa hawa sehemu mbali mbali za Bara la Afrika na nje ya Afrika. Itakumbukwa kwamba, Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa, lilianzishwa kunako mwaka 1941 kwa lengo la kuwasaidia Wamissionari kutekeleza shughuli za kichungaji, Jimbo kuu la Mombasa.

Hadi sasa Shirika hili lina jumla ya watawa 270 wanaotekeleza utume wao kwa njia ya kufundisha katekesi, kuhudumia wagonjwa, kufundisha shuleni na kwa namna ya pekee kuwahudumia watoto yatima na wagonjwa wa Ukimwi. Hili ni Shirika linaloongozwa na karama na moyo wa Kibenediktini, kwa kuzingatia kanuni msingi ya: Sala na kazi: "Ora et Labora".

Ni sala inayowawezesha watawa hawa kujipatia nguvu ya kuweza kuwahudumia watu kiroho na kimwili na kwamba, kwa njia ya kazi za mikono yao wanajipatia mahitaji yao msingi kama sehemu ya mchakato wa kujitegemea na kuendelea kutekeleza utume na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.