2014-07-24 16:09:19

Machimbo ya dhahabu kweupee! Yaani we acha tu!


“Nchi yetu imekalia hazina tele, yaani inayo akiba ya madini ya dhahabu wakia milioni 36. Kuna Almasi kedekede, kuna mawe ya thamani kibao, mafuta tani nyingi sana, mkaa umezagaa nk. Upatikanaji na uchimbaji wa hazina hizo ni wa aina mbili: Mosi, kuna wachimbaji wadogo wadogo wanaobahatisha.


Pili, kuna kampuni kubwa zinazowekeza kwenye uchimbaji. Mara zote faida ya uchimbaji huo inaingia mfukoni mwa mchimbaji mwenyewe. Hazina ndiyo hiyo! Ninawaalika kuchangamkia masuala. Kabla ya kuanza kukurupuka kwenda machimbo, hebu jipatie semina fupi ya mbinu za upatikanaji wake. Usipozingatia semina hii usishangae badala ya kurudi na hazina toka machimboni, litarudi jina tu bila wewe mwenyewe.”


Suala la utafutaji hazina iliyofichika ardhini na la wachimbaji wadogowadogo na la wawekezaji wakubwa ni la toka enzi hata kabla ya Yesu. Leo Yesu anapenda kuwatolea semina fupi wachimbaji wadogowadogo, na kwa wawekezaji wa migodi, namna ya upatikanaji wa hazina hiyo. Usishangae Yesu anapoanza na mifano pacha inayohusu hazina na lulu akizilinganisha na ufalme wa mbingu. Mifano hii ni pacha kwa vile ina ujumbe mmoja lakini kila mmoja una jambo fulani la pekee.


Mfano wa kwanza, Yesu anasema kuwa ufalme wa mbingu ni sawa na hazina iliyofichika shambani. Hilo lilikuwa ni jambo la kawaida la mtu kugundua hazina zilizofichwa mashambani. Hazina hizo zilikuwa zinafichwa wakati wa kukimbia vita wakitegemea kuja kuzitumia tena warudipo baada ya vita. Kwa bahati mbaya mara nyingi wakazi hao walishindwa kurudi tena makaoni kwao, na itokeapo labda mmoja anapitapita humo na kuona kitu kinang’aa anakifuatilia na anagundua kuwa ni hazina iliyofichwa. Yasemekana kwamba katika mji wa Nazareti kulikuwa na watu tajiri walioishi, miaka elfu mbili kabla ya Kristu hadi wakati wa Nabukodonosor. Baadaye mji huo ukafutika wote wakati ulipobomolewa pamoja na mji wa Yerusalemu sababu ya vita.


Hivi mji huo wa Nazareti haukuwepo hadi miaka mia mbili kabla ya Kristu ndipo ulipoanza tena kukaliwa na watu. Kwa hiyo, yawezekana watu walipokuwa wanautoroka mji huo wakaficha hazina kwenye mashamba yao, ndiyo maana sasa wakawa wanabahatika kuzigundua wanapotaka kuanza kujenga. Mfano mwingine ulikuwa ni nyumba ya kifahari ya Megido ilijengwa kwa pembe za ndovu tu. Hapo kulikuwa na wakazi kati ya miaka 1550 hadi 1150 kabla ya Kristu, walipopanganika kutoroka wakati wa vita wakafukia ardhini kilo nyingi sana za pembe na vitu vingine vya thamani, kwa bahati nzuri wevi na watu wengine hawakuweza kuvivumbua hadi pale wana-akiolojia yaani watafiti wa mabaki ya kihistoria walipofanya utafiti wakazigundua.


Mfano wa pili ni ule wa mtafutaji wa Lulu, kwa kigiriki inaitwa gema au kwa kiyahudi ni penina. Kwa watu wa mashariki Lulu iliwakilisha uzuri. Jina la kihebrani Penina ni jina walilopewa zaidi wasichana kuonesha uzuri. Katika Biblia tunamkuta Elkana baba ya Samweli alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana, na wa pili aliitwa Penina (I Sam 1:2). Si ajabu kuona wasichana wengi wa kiswahili wakiwepo wasanii wanapenda kuitwa Lulu kuonesha uzuri.

Kwa kawaida mwanaume anamzimikia mwanamke mzuri – yaani lulu. Duniani kitu kizuri (lulu) kinatafutwa. Lakini hapa uzuri au ubaya tunaoumaanisha siyo ule wa sura au wanavyoita “reception imekubali au reception haijakubali” la hasha, bali wabaya ni wale waovu kwa ndani, yaani wabinafsi, wasiosogeleka, wakali, walipa kisasi. Watu aina hiyo tunasema siyo wazuri. Neno nzuri, Habari njema au Lulu nzuri kupita zote ni Yesu wa Nazareti. Huyo kweli ni mzuri, huyu ndiye Lulu pekee. Yaani Yesu ni mtu anayejali wengine, anayeheshimu, anayependa, anayewasaidia, anawasikiliza, huyo ni lulu kweli. Hapo mtafutaji wa uzuri anapoikuta lulu aina hii anawania kuipata kwa kuuza kila kitu ili ainunue.

Lakini budi tuelewane toka mwanzo kuwa wahusika wakuu wa mifano hii siyo watu hawa wawili, bali ni haya machimbo ya hazina na lulu. Kutokana na hoja kwamba, nguvu na msisitizo wote umewekwa katika kuvitafuta vitu hivyo, na hasa katika furaha inayoweza kupatikana baada ya kuipata hazina inayotafutwa. Kama furaha ya mchimbaji mdogo anapobahatika kupata kipande cha dhahabu baada ya kuchekecha udongo kwa mwezi nzima bila kupata kitu.


Katika nafasi hii, kama anavyosema Yesu kuwa hazina na lulu hizo, ni ufalme wa Mungu au Yesu Kristu mwenyewe. Hazina hiyo yaweza kugunduliwa kwa bahati au pengine kwa kuwaniwa hasa kwa njia ya kuitafuta, ya kutafutwa na mtu ambaye labda hajaridhika na maisha na anatafutatafuta maisha yanayoweza kutosheleza hamu yake, ndipo anakuja kugundua hazina ambayo ni Yesu Kristu.


Baada ya kuigundua hazina na lulu yake ndipo unasikia lugha kama hii: “Wewe ni hazina yangu, Wewe ndiye lulu, wewe ni furaha ya moyo wangu, wewe ni upendo wangu, wewe ni almasi ya maisha yangu, nk lugha kama hii ni ya kawaida kwa wapendanao. Kwa hiyo imani katika Kristu, ni kwa yule anayependa anapogundua mtu wa kupendwa na anayoweza kumwaminia na kukabidhi maisha yake.


Katika mfano wa hazina ambayo mmoja anaweza kuigundua kwa bahati tunaweza kumtaja Petro. Huyu aliigundua kwa bahati hazina hiyo ambayo ni Kristu. Kukutana kwa Yesu na Petro kulitokea kwa bahati tu, kwani chanzo ni Andrea kaka ya Petro, aliyeonana na Yesu wakati wa ubatizo wa Yohane, akaenda kumsimulia Petro na kumjulisha kwa Yesu. Kwa bahati naye Petro mara mmoja akaamua kumfuata Yesu.


Iko mifano mingi ya watu wanaomgundua Kristu halafu mara moja wanaamua kumfuata, kama ilivyo kwa mchimbaji huyu wa hazina. “Kutokana na furaha yake anaenda kuuza kila kitu ili kununua shamba nzima.” Yaonekana kuwa mtu huyu aligundua sehemu tu ya hazina na akaamini kwamba kutakuwa na uhondo zaidi wa hazina, hata kaamua kwenda kuuza kila kitu ili aweze kununua shamba lile lote. Ndivyo ilivyo kwa yule anayemgundua Kristu atakuwa ameona baadhi tu ya mambo ya thamani na sehemu tu ya mapendekezo mazuri ya Yesu, ila atakuwa anajua pia kwamba Kristu huyo anayo hazina kubwa zaidi atakayogundua polepole katika kumfuata.


Kadhalika msichana aliyemzimikia mvulana, anaamini kwamba kijana huyo anayo mapaji au hali anayoiaminia, lakini ataigundua katika maisha akimfuata. Baada ya kugundua hazina hiyo, mtu anaenda kuuza kila kitu. Aidha kuhusu furaha ipatikanayo, hiyo ni furaha aionayo mtu baada ya kuigundua hazina. Katika maisha inatakiwa kutolea sadaka na kuachana na uwongo, kujaribia, ujasiri, mapendeleo, lengo lakini ni furaha itokanayo na kugundua hazina. Mfuasi au mtume wa kweli hazungumzi zaidi juu ya kile alichokiacha, bali huzungumzia zaidi juu ya kile alichokigundua, kile alichokipata.


Hofu yetu ni kupoteza maisha. Kwa sababu Mapendekezo anayotoa Yesu huoni mara moja mapato yake. Hapa huzungumzia furaha mfano wa kijana tajiri anapopendekezewa kuacha yote na kumfuata Yesu, kijana anaondoka huku amehuzunika kwa sababu hakuelewa hazina aliyoikuta kwa bahati pale. Hakujiamini kuacha yote kusudi kufuata hazina iliyofichika katika kumfuata Yesu. Kumbe aliyeigundua hazina au lulu inabidi mara moja atoe uamuzi wa kuichukua au kuiacha. Kama vile katika kupendana, endapo mmoja amependa, asipoteze muda na nafasi. Hivi ndivyo katika maisha ya kikristu mmoja aliyemgundua Kristu yabidi kuchukua uamuzi mara moja wa kumfuata.


Mfano wa mwisho ni ule wa wavu uliotupwa baharini unaozoa kila takataka. Baada ya kujaa wavuvi huvuta ufuoni na kuchaguzi. Mwishoni mwa ulimwengu wanatenganishwa wema wanapelekwa paradisini na wabaya hutupwa motoni. Taarifa hii yaweza kutafsiriwa vibaya. Ili kuelewa vizuri sehemu hii ni kwamba yule mtu au nafsi mbaya na nzuri iko katika mimi huyu. Habari njema ni kwamba ule upande mbaya wa mimi utashindwa na kuunguzwa na upendo wa Mungu. Hivi ule upande mbaya wa mimi utajisikia umeshindwa, na utajijutia, wakati ule upande mzuri wa mimi ndiyo utakaofurahi katika ufalme wa Mungu.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.