2014-07-24 16:12:00

Gaza- Ghasia haziwezi kufanikisha ushindi


Askofu Mkuu Silvano Maria Tomasi , Mtazamaji wa kudumu wa Jimbo la Papa katika Ofisi za Umoja wa Mataifa za mjini Geneva, Jumatano alitoa mchango wa Jimbo la Papa , katika kikao cha 21 cha Baraza Maalum la Haki za Binadamu juu ya hali ya haki za binadamu , Palestina na Yerusalemu ya Mashariki.

Mchango wa Askofu Mkuu Silvano ulisisitiza ukweli kwamba, hakuna atakayekuwa mshindi kwa kutumia ghasia. Wakati idadi ya watu wanaouawa, kujeruhiwa na kukimbia makazi, inaendelea kuongezeka katika mgogoro huu kati ya Israel na vikundi vya baadhi ya Wapalestina, hasa katika Ukanda wa Gaza, sauti yenye hoja inazidi kudidimizwa na milio ya silaha. Mipango ya vurugu, haitawafikisha popote iwe kwa sasa au kwa siku za baadaye.

Askofu Mkuu Silvano aliendelea kuonya kwamba, ukosefu wa haki, hasa ukosefu wa haki ya kuishi kwa amani na usalama, hauna lolotejema isipokuwa hupanda mbegu mpya ya fitina na chuki. Ni kuimarisha tu utamaduni wa unyanyasaji , ambao matunda yake ni uharibifu na kifo, kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa muda wote wa mgogoro huu wa muda mrefu, katika ukanda wa Gaza.Miaka yote ya ghasia , hakuna mshindi zaidi ya majanga, mateso na vifo. Na Wengi wa waathirika ni raia, ambao kwa mujibu wa sheria ya kibinadamu ya kimataifa,wanapaswa kulindwa.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takriban asilimia sabini ya Wapalestina wanaouawa ni raia wasiokuwa na hatia, kama ilivyo pia upande wa Israel, ambako makombora ya Palestina yamekuwa yakielekezwa kwa raia wa Israel. Dhamiri za raia wema wa maeneo hayo, zimepoozwa na hali hii ya machafuko ya muda mrefu, ambayo kwa sasa yanaonekana kutaka kulazimisha , ufumbuzi kwa njia ya maangamizo mengine. Ni vyema wote kukumbuka kwamba, kupandisha hasira wengine , hakuwezi kuondoa haki za watu hao. Badala yake, inafaa kutumia njia ya haki kwa ajili ya sasa na kwa siku za usoni, kutambua ubinadamu wa mtu na haki zake kawaida.

Baba Mtakatifu Francisco, katika ziara yake kitume kwa Nchi Takatifu,Mei mwaka huu, alisisitiza kwamba, hali ya sasa, kati ya Israel na Palestina, haikubaliki , na hivyo ni lazima kupata suluhu kufikisha mwisho mgogoro uliopo. "Kwa manufaa ya wote," alisema, "kuna haja ya kuongeza jitihada na mipango kwa lengo la kujenga mazingira ya amani yaliyo thabiti kwa mujibu wa msingi wa sheria, na utambuzi wa haki ya kila mtu binafsi, na juu ya usalama wa pande zote"." Wakati umefika kwa kila mtu kupata ujasiri wa kuwa mkarimu na mbunifu katika huduma kwa manufaa ya wote. Ujasiri wenye kuchipusha amani ambamo wote wanakiri na kutambua haki za wote katika mataifa yote mawili, Israel na Palestina. Papa alisisitiza uwepo wa maisha yenye amani na salama ndani ya mipaka inayo tambuliwa kimataifa, ikiwa pamoja na mazingira bora ya maisha, na upatikanaji wa huduma za kawaida, kama madawa, maji na ajira, ambavyo bila ya kuzingatia haki za kibinadamu. Alisema bila amani ni vigumu sana kuwa na maendeleo na ustawi endelevu.


Ujumbe wa Jimbo la Papa , ulikamilisha kwa kurudia mtazamo wake kwamba, vurugu kamwe hazilipi. Vurugu husababisha tu mateso zaidi, uharibifu na kifo, na huzuia watu kuyafurahia maisha katika haki na ukweli wake. Na umevitaka Vyombo vya habari , kutoa taarifa za kweli na katika haki bila ya kupendelea upande wowote na hasa iwe kwa lengo la kuwezesha maendeleo katika majadiliano yasiyo na upendeleo, bali kwa ajili ya kujenga utambuzi wa haki kwa kila mtu, heshima na faida zinazo tokana na mshikamano wa jumuiya ya kimataifa katika kusaidia jitihada kubwa kufikia amani.
Jimbo la Papa limeonya ,udumishaji wa mduara wa kulipiza kisasi, unakuwa kitisho zaidi kwa siku za usoni. Watu, wanaume kwa wanawake wataendelea kuishi kama maadui na wapinzani, ambapo wakiwa na amani, wanaweza kuishi kama marafiki, kaka na dada, wakiinua kihali na kiroho pia. .









All the contents on this site are copyrighted ©.