Askofu Giorgio Bertin wa Jimbo Katoliki la Djibouti na Msimamizi wa kitume wa Jimbo
kuu la Mogadisho, Somalia anasema, yataka moyo kweli kweli kuwa Mkristo nchini Somalia
na kusimama kidete ili kuwa ni sauti ya wanyonge, kwa kutetea utu na heshima ya binadamu.
Ukijifanya kutekeleza dhamana ya Kanisa kwamba ni sauti ya wanyonge, ukafumbwa mdomo
na kuamriwa kuondoka nchini Somalia kwa mwendo wa kunyakua!
Askofu Bertin ambaye
tangu mwaka 2001 anaishi na kutekeleza utume wake Jimboni Djibouti anasema, hali ni
shwari kwa kiasi fulani. Serikali inaonekana kutekeleza wajibu wake wa ulinzi na usalama
na kwamba, wananchi wa Djibout wanaliheshimu na kulipenda Kanisa. Kutokana na woga
uliofichika katika mioyo ya watu, kunaonekana kana kwamba, kuna amani na utulivu,
lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba, watu ni waoga kudai haki zao msingi, kwani
wanahofia kufungwa mdomo na kutoweka katika uso wa dunia.
Takwimu zinaonesha
kwamba, Wakristo ni asilimia 6% ya idadi ya wananchi wa Djibouti na wengine wote ni
waamini wa dini ya Kiislam, changamoto kubwa ni kuendeleza majadiliano ya kidini,
ili kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na udugu kati ya watu.
Umaarufu
wa Kanisa unatokana na huduma makini zinazotolewa na Kanisa katika sekta ya elimu,
afya na maendeleo ya watu: kiroho na kimwili. Serikali imeridhishwa na mchango wa
Kanisa katika sekta ya elimu kiasi kwamba, imeridhia kulipa mishahara ya walimu kwa
shule nne zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa kama alama ya shukrani kwa mchango
wa Kanisa katika maendeleo ya wananchi wa Djibouti. Inasikitisha kuona kwamba, kiwango
cha miito ni duni sana, kiasi kwamba, Jimbo linahudumiwa kwa kiasi kikubwa na Mapadre
kutoka nje ya nchi.