2014-07-23 10:41:46

Changamkieni mitandao ya kijamii katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya!


Askofu Bernadin Francis Mfumbusa, Mwenyekiti wa Idara ya Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akiwasilisha mada kuhusu athari za teknolojia ya digitali na njia za mawasiliano ya jamii katika maisha na utume wa Kanisa, amewataka Wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA wanaohudhuria mkutano wao wa kumi na nane, unaoendelea mjini Lilongwe, Malawi, kuvalia njuga matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya Barani Afrika.

Askofu Mfumbusa ameitaka mihimili ya Uinjilishaji Mpya kujifunza kwa bidii na kuanza kutumia mitandao ya kijamii katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, vinginevyo wanaweza kujikuta wamepitwa na wakati na watu wanaowahudumia. Watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kubadilishana habari na kushirikishana ujuzi na maarifa na kwamba, kuna idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao hii katika Jamii. Kumbe, matumizi ya mitandao ya kijamii, si jambo la hiyari tena, bali watu wanapaswa kucharika ili kuhakikisha kwamba, wanatumia mitandao ya kijamii.

Askofu Mfumbusa amewataka Maaskofu wa AMECEA kuhakikisha kwamba, somo la teknolojia ya mawasiliano ya jamii linaingizwa katika mitala ya masomo ya Seminarini na katika nyumba za malezi, ili kuwajengea Majandokasisi uwezo wa kutumia mitandao hii tangu awali Ikiwa kama Kanisa litashindwa kujipyaisha kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, anasema Askofu Mfumbusa, litashindwa pia kutekeleza agizo la Yesu kwenda ulimwenguni kote kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu.

Kwa kutumia mitandao ya kijamii, Kanisa linaweza kwenda mbali zaidi kwa muda mfupi na kwa njia hii, Kanisa linaweza kujenga Parokia na Majimbo kwenye mitandao ya Kijamii. Askofu Mfumbusa ameyashauri Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuwa na sera makini za mawasiliano ya jamii zitakazoyawezesha watu kupata habari.

Mikakati hii haina budi kwenda sanjari na majiundo makini ya viongozi na wafanyakazi wa Kanisa katika masuala ya mawasiliano ya kijamii, kwani wengi wao bado wako nyuma sana. Amewashauri Maaskofu wa AMECEA kuandaa semina zitakazosaidia kuwahamasisha watu kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii

Naye Askofu James Maria Wainaina wa Jimbo Katoliki Murang'a, Kenya akipembua kuhusu Liturujia na Utamadunisho kama njia za Uinjilishaji Mpya, amewataka wajumbe wa AMECEA kuendeleza dhana hizi mbili kwani ni sehemu ya utambulisho wa waamini katika Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Lakini waamini watambue kwamba, maadhimisho ya Liturujia ni kazi na wajibu wa Yesu Kristo, Kuhani mkuu, dhamana inayoendelezwa na Mapadre katika Liturujia, ili Mwenyezi Mungu atukuzwe na binadamu atakatifuzwe.

Kanisa Barani Afrika linapaswa kuwa na mchakato maalum wa utamadunisho, ili kugusa undani wa maisha na vipaumbele vya watu na wala si kwa kucheza ngoma, au kubadili mtindo wa mavazi yanayotumika katika Ibada mbali mbali za Kanisa. Maaskofu wanashauriwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati mwongozo uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia na Maelekezo ya kina yaliyochapishwa na Baraza la Kipapa la Sakramenti na Nidhamu ya Kanisa kunako mwaka 1994.

Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, Tanzania, katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wajumbe wa AMECEA, Jumanne, tarehe 22 Julai 2014, amewataka waamini kuwa imara katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake. Wajitahidi kuiga mfano wa Maria Magdalena aliyebaki mwaminifu kwa Kristo hata baada ya kuteswa, akafa na hatimaye, akapewa dhamana ya kwenda kushuhudia ufufuko wa Kristo kwa Mitume wa Yesu.

Waamini wajitahidi kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia katika: Liturujia ya Neno na kwa njia ya kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa. Waamini wajifunze utamaduni wa kumsikiliza Kristo kwa umakini mkubwa kwani Yeye ni Bwana na Mwalimu wa nyakati zote. Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, Wakristo wote wanahamasishwa kuwa ni vyombo vya utangazaji wa Injili ya Furaha kwa Watu wa Mataifa pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati.







All the contents on this site are copyrighted ©.