2014-07-18 12:07:28

Salam na matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam!


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini limewatumia ujumbe wa matashi mema waamini wa dini ya Kiislam katika maadhimisho ya Siku kuu ya Id Al Fitr inayokuja mara baada ya Mfungo mkutukufu wa Mwezi wa Ramadhani, kipindi cha kufunga, swala na msaada kwa maskini.

Mwaka 2013, Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro aliandika ujumbe wa matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam katika maadhimisho ya Siku kuu ya Id Al Fitr kuonesha upendo na mshikamano wake kwa waamini wa dini ya Kiislam kama ndugu, maneno ambayo yana maana sana! Hii inatokana na ukweli kwamba, Waislam na Wakristo ni ndugu wamoja wanaounda Familia moja ya binadamu iliyoumbwa na Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo.

Waamini wa dini hizi mbili kwa pamoja wanaungama imani kwa Mungu mmoja Muumbaji wa binadamu na kwamba, wanautukuza ukuu wa Mungu kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Wanamwabudu na kujiweka miguuni pa Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kuthubutu kuitana ndugu katika imani kwa Mungu mmoja. Ni maneno yaliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1982 alipokutana na viongozi wa kidini mjini Kaduna, Nigeria.

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini linasema, kwa pamoja waamini wa dini hizi mbili wanamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mambo yale yanayowaunganisha pamoja na kutambua tofauti zao msingi. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini yanayojikita katika hali ya kuheshimiana pamoja na urafiki; kwa kusimamia tunu msingi za udugu, ili kwa pamoja waweze kufanya kazi ya kuendeleza haki na amani; kwa kuheshimu utu na haki msingi za kila binadamu.

Wakristo na Waislam wanatambua kwamba, kimsingi wanawajibika kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii: wagonjwa, yatima, wahamiaji, wahanga wa biashara haramu ya binadamu, waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia. Masuala yote haya ni changamoto kubwa katika kujenga na kudumisha mshikamano miongoni mwa watu wenye mapenzi mema. Ni changamoto inayotishia uharibifu wa mazingira, myumbo wa uchumi kimataifa na ukosefu wa fursa za ajira na hasa zaidi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Mambo haya yanawafanya watu kunyong'onyea kiasi cha kukosa matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Waamini hawawezi kamwe kusahau matatizo yanayoziandamana familia kwa kutengana na kuwaacha watoto wadogo katika shida na mahangaiko makubwa. Kumbe, kuna haja ya kufanya kazi kwa pamoja, ili kujenga madaraja ya amani na upatanisho hasa katika maeneo ambayo Waislam na Wakristo ni wahanga wa vita. Urafiki kati ya waamini wa dini hizi mbili usaidie mchakato wa ushirikiano ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali kwa ajili ya mafao ya wengi.

Upatanisho, haki, amani na maendeleo ni kati ya vipaumbele vya waamini wa dini hizi mbili kwa ajili ya mafao ya Familia ya binadamu. Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, likiwa limeungana na Baba Mtakatifu Francisko linapenda kuwapatia salam na matashi mema waamini wote wa dini ya Kiislam katika Siku kuu ya Id al Fitr; heri, fanaka na amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.