Utamaduni unaosimikwa katika ubinafsi na uchoyo ni kati ya mambo yanayochangia kuporomoka
kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kumbe, kuna haja kwa Mama Kanisa kujifunga
kibwebwe kuhakikisha kwamba, Familia inapewa kipaumbele cha kwanza katika mikakati,
maisha na utume wa Kanisa.
Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni
na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia wakati wa maadhimisho
ya mkutano mkuu wa kumi wa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati,
ACERAC lililokuwa linakutana huko Brazzaville, Congo.
Askofu mkuu Paglia anasema,
Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi kuhusiana na maisha na utume wa Familia,
kiasi cha kupindisha hata mpango na utashi wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Hii
ni changamoto ya kiimani na kimaadili inayopaswa kufanyiwa kazi kwa kina na mapana,
ili kujikita katika maendeleo ya kweli yanayoheshimu misingi ya utu na heshima ya
binadamu.
Kuna mmong'onyoko mkubwa wa tunu bora za kimaadili na utu wema;
umoja, upendo na mshikamano katika maisha ya ndoa kwa sasa uko mashakani kutokana
na ubinafsi na kwamba, ule mshikamano wa kifamilia uliokuwepo Barani Afrika kwa miaka
mingi unaendelea kuyeyuka kwa kasi kubwa.
Tatizo jingine linaloibuka kwa sasa
ni ukosefu wa uaminifu katika maisha ya ndoa na familia, kiasi kwamba, kuna baadhi
ya wanandoa wanadhani "kuchepuka" ni suluhu ya matatizo wanayokabiliwana nayo katika
ndoa zao, kumbe, hapa wanaendelea kujichumia majanga binafsi na kwa ajili ya familia
zao. Umaskini na ukosefu wa fursa za ajira ni changamoto kubwa kwa familia nyingi
Barani Afrika, kiasi cha kuwafanya wazazi na walezi kushindwa kutekeleza dhamana kwa
familia zao.
Ikumbukwe kwamba, Familia Barani Afrika daima imekuwa ni shule
ya kwanza katika kurithisha tunu msingi za maisha ya imani, maadili na utu wema, lakini
kwa sasa dhamana hii iko hatarini kupokwa na vyombo vya mawasiliano ya kijamii!
Askofu
mkuu Paglia anasema, umefika wakati kwa familia kujenga na kuimarisha misingi ya ndoa
na familia; kwa kukuza mahusiano bora ndani ya Jamii, ili kujenga mshikamano wa upendo
kati ya wazee, vijana na watoto. Hii ni changamoto ya Kanisa zima na wala si tu kwa
ajili ya Kanisa Barani Afrika.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua fursa,
changamoto na kinzani zinazoendelea kuiandama Familia, ameamua kuitisha Sinodi maalum
ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 5
hadi tarehe 19 Oktoba 2014. Kutakuwepo na awamu ya pili ya maadhimisho haya itakayofanyika
mwaka 2015.
Hii ni changamoto kwa Serikali, taasisi, wanasiasa, wachumi na
watunga sera kufuata mfano wa Kanisa Katoliki katika kulinda, kutetea na kudumisha
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Familia iwe ni kiini cha mawazo na sera
makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.