2014-07-16 08:38:41

Hakuna uhusiano wowote kati ya imani na matumizi ya nguvu!


Katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2009- 2014, Tume ya Taalimungu Kimataifa imefanya tafakari na upembuzi wa kina kuhusu Mwenyezi Mungu kadiri anavyofundishwa na Kanisa. Tume ikajiuliza swali msingi kama kuna uhusiano wowote kati ya Imani kwa Mungu mmoja na matumizi ya nguvu. RealAudioMP3

Tafakari hii imefanyika katika makundi mbali mbali na hatimaye, ikajadiliwa kwa kina na mapana na Tume hii katika mikutano yake mikuu na hatimaye, kufikia uamuzi ambao matokeo yake yalipelekwa kwa Kardinali Gerhard L. Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na kuidhinisha kwamba, hati hii: “Mwenyezi Mungu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na Umoja wa binadamu: Ukristo katika Imani ya Mungu mmoja dhidi ya vitendo vya nguvu.”

Huu ni utafiti unaohitaji kupatiwa majibu muafaka mintarafu uelewa wa kitaalimungu kwani kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, kuna uhusiano wa karibu kati ya Imani kwa Mungu mmoja na vita vya kidini; matukio ambayo yamekuwepo katika historia ya mwanadamu. Huu ni uelewa potofu wa Mafundisho ya Kikristo kuhusu Imani kwa Mungu mmoja.

Tafakari hii inaweza kufupishwa kwa kujiuliza maswali msingi; Je, taalimungu ya Kikatoliki inaweza kujibu kwa ufasaha na kwa kiasi gani katika changamoto za kitamaduni na kisiasa zinazotaka kuunganisha Imani kwa Mungu na mmoja na vita ya kidini? Je, ukweli wa kiimani kuhusiana na Mungu mmoja unaweza kutambulika kuwa ni nguzo na chemchemi ya upendo kati ya binadamu?

Majibu ya maswali haya msingi ni tafakari ya kina inayojikita katika ushuhuda wa maisha kwa kukubaliana kimsingi kwamba, vita ya kidini kwa kisingizio cha kutaka kueneza Imani kwa Mungu mmoja ni mwelekeo potofu wa kidini mintarafu uelewa wa Kikristo uliofikia kilele chake kwa njia ya ufunuo wa Yesu Kristo. Kanisa linatambua kwamba, ushuhuda wa Imani unajikita kwa namna ya pekee katika toba na wongofu wa ndani, jambo linalohitaji tafakari na uchunguzi wa dhamiri ya mtu binafsi.

Sura ya kwanza yaWaraka wa Tume ya Taalimungu Kimataifa inafafanua maana ya Imani kwa Mungu mmoja kama inavyoeleweka katika misingi ya falsafa ya kisiasa kwa nyakati mamboleo. Wanatambua mabadiliko makubwa yaliyofikiwa hadi hadi sasa: kutoka katika dhana ya ukanimungu hadi kufikia nyakati hizi ambako kuna uelewa potofu wa Imani na siasa zinazotaka kung’oa uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Maana ya Imani kwa Mungu mmoja ni jambo muhimu sana katika utamaduni mamboleo na kwa watu wanaoamini katika Mungu mmoja yaani: Wayahudi, Waislam na Wakristo. Tume inafanya upembuzi yakinifu kwa kukataa katu katu matumizi ya nguvu kwa ajili ya kuunga mkono dhana ya Imani kwa Mungu mmoja wala kukubaliana kimsingi na siasa zinazotaka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa maisha ya mwanadamu na vipaumbele vyake. Kimsingi wanakubaliana na waamini na wale wasioamini kwamba, vita vya kidini ni dhana potofu na iliyopitwa na wakati.

Kama Wanataalimungu wa Kikatoliki wanatambua kwamba, Yesu kristo aliwafunulia wafuasi wake uhusiano wa upendo kati ya Mungu na mwanadamu, jambo msingi katika ufahamu wa Imani kwa Mungu mmoja na kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Yesu Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Katika Sura ya Pili, Tume inaangalia sehemu za Maandiko Matakatifu ambazo ni ngumu kueleweka kwa urahisi. Hizi ni sehemu ambazo ufunuo wa Mwenyezi Mungu unajionesha kwa namna ya pekee na matumizi ya nguvu dhidi ya binadamu. Sehemu hizi zinafafanuliwa na vifungu vingine vya Neno la Mungu kama tafsiri sahihi ya Neno la Mungu. Kwa kuwa na msingi huu, Tume inaendelea kupembua mwelekeo wa kibinadamu na Kikristo katika kufafanua tafsiri hii mintarafu matukio ya kihistoria.

Kwenye Sura ya Tatu, Tume inafanya tafakari ya kina kuhusu uelewa wa Fumbo la Pasaka, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo, kama nguzo msingi ya upatanisho kati ya mwanadamu. Kazi ya ukombozi ni muhimu sana katika kutoa ufafanuzi wa kitaalimungu. Ufunuo unaojionesha katika tukio la maisha ya Yesu Kristo, linalomfunulia binadamu upendo na huruma ya Mungu, unaonesha ukweli wa mafundisho juu ya Kristo na Ukweli wa Fumbo la Utatu Mtakatifu dhidi ya vita vya kidini.

Na katika Sura ya Nne, Wanataalimungu wa Kimataifa wanaelezea kwa kina na mapana mawazo juu ya Mwenyezi Mungu mintarafu uelewa wa kifalsafa. Wanachambua mawazo ya watu wasiomwamini Mungu pamoja na uelewa wa watu wasiokuwa na misimamo thabiti ya kidini. Ufafanuzi hii unaendelea kujikita katika majadiliano ya kidini kwa kuonesha uhusiano uliopo kati ya dini zinazoamini katika Mungu mmoja. Mwishoni wanatoa tafakari ya kina inayojikita katika misingi ya kifalsafa na kitaalimungu kuhusu Ufunuo na uhusiano wake kwa uelewa wa Mungu katika Mapokeo na hali ya kawaida.

Sura ya Tano na ya Mwisho katika Hati hii kutoka Tume ya Taalimungu Kimataifa inatoa muhtasari wa mambo msingi yanayokaziwa na Mama Kanisa katika mchakato wa ushuhuda wa upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu; na binadamu wao kwa wao. Ufunuo wa Kikristo unasafisha dini, kwa kumweka mwanadamu mahali pake katika mchakato wa kutafuta maana ya maisha. Ni jambo la maana sana ikiwa kama masuala ya kitaalimungu yataweza kufafanuliwa kadiri ya maendeleo na historia ya ufunuo wa Mwenyezi Mungu kadiri ya ufahamu wa Kikristo.

Muhtasari huu umetarishwa na
Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.