2014-04-23 09:16:27

Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II wanashiriki utakatifu mmoja!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, utakatifu ni wito na changamoto kwa kila mwamini na kwamba, wote wanaitwa kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II ni viongozi wa Kanisa waliojitahidi kutekeleza utakatifu mmoja, kwa njia ya nyajibu zao, huku wakiongozwa na Roho wa Mungu, kwa njia ya utii na ibada katika roho na kweli!

Miamba hawa wa Kanisa walijitahidi kumfuasa Yesu Kristo: mtii,fukara na mnyenyekevu aliyeonesha njia ya utakatifu wa maisha kwa Fumbo la Msalaba, ili aweze kuwastahilisha kushiriki utukufu wake. Hawa ni watu ambao kwa njia ya ushuhuda wa imani hai na tendaji, walionesha imani, matumani na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake.

Askofu mkuu Vincenzo Bertolone wa Jimbo kuu la Cantanzaro- Squillace, Italia ndivyo anavyochambua utakatifu wa Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II; viongozi wakuu wa Kanisa waliojitahidi kusoma alama za nyakati na hivyo kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni viongozi waliojitahidi kudumisha majadiliano na walimwengu kwa njia ya mwanga na kweli za Kiinjili, ili kumpeleka Kristo kati ya watu na watu kwa Kristo.

Watu mbali mbali walishuhudia na kuonja utakatifu wa maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; uhuru wa kweli; haki, amani na maendeleo ya binadamu. Alivunjilia mbali kuta za utengano kati ya watu na leo hii anakumbukwa kuwa ni kati ya viongozi waliosambaratisha ukomunisti duniani.

Mwenyeheri Yohane Paulo II alilitaka Kanisa kujikita katika Uinjilishaji Mpya, ili watu wanaotembea katika mwanga na kweli za Kiinjili waweze kutolea ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake. Alikazia na kusisitiza umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Alionesha kwamba, hakuna ukinzani wala mpasuko kati ya imani na uwezo wa mwanadamu wa kufikiri na kutenda, bali jambo la msingi ni kutambua na kukiri uwepo wa Mungu ambaye ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho wa yote!

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, anakumbukwa na wengi kwa kuhimiza utakatifu wa maisha ya ndoa na familia na kwamba, Familia za Kikristo zinapaswa kuwa kweli ni shule ya utakatifu, haki na amani; upendo na mshikamano. Hapa ni mahali pa kwanza ambapo mwanadamu anajifunza tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakizingatia dhamana na utume wa Familia, wanaweza kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia kwa ujasiri na moyo mkuu!







All the contents on this site are copyrighted ©.