Maelfu ya waamini pamoja na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, asubuhi na
mapema siku ya Jumatano tarehe 23 Aprili 2014, waliwahi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu
la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kusikiliza katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko
wakati huu wa Kipindi cha Pasaka. Baba Mtakatifu katika katekesi yake ameuliza swali
la msingi "kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?
Baba Mtakatifu Francisko
anasema, furaha ya Siku kuu ya Pasaka inapata chimbuko lake katika imani kwa Ufufuko
wa Yesu Kristo sanjari na uwepo wake endelevu ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu.
Kwa njia ya Ufufuko, yote yamefanywa kuwa upya. Swali ambalo wanawake waliulizwa siku
ile ya Pasaka ni swali ambalo Mama Kanisa anapenda kuwaswalisha watoto wake, kwa nini
mna mtafuta aliye hai katika wafu?
Baba Mtakatifu anasema, Injili inatoa mifano
mitatu ya watu waliokutana na Yesu, wakaonja mabadiliko katika maisha yao ya kiroho,
mwaliko na changamoto hata kwa waamini wa nyakati hizi. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu
Toma, waamini wana shauku ya kutaka kuona ukweli wa maisha mapya yanayobubujika kutoka
kwa Kristo mfufuka. Kama ilivyokuwa kwa Maria Madgalena, waamini wanapenda kusikia
sauti ya Yesu Mfufuka ikiwaita kwa majina yao!
Baba Mtakatifu Francisko anasema
kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emmaus waliokuwa wanasafiri, waamini pia wanataka
kuonja furaha na matumaini mapya kwa kutambua kwamba, Yesu anaendelea kutembea pamoja
nao. Wafuasi wa Emmaus walikuwa wanafikiri uwepo wa Yesu kati ya wafu, akawaongoza
kwa njia tofauti katika imani na nguvu yake ya ufufuko.
Leo hii, waamini wanachangamotishwa
kumtafuta Yesu aliyefufuka kutoka katika wafu kwa kuachana na mambo yote ambayo ni
kizingiti cha kutaka kukutana na Yesu, ili kupata maisha mapya, uhuru wa kweli unaoweza
kutolewa na Yesu mwenyewe.
Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Mashemasi wapya
kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Ireland waliokuwa wameambatana na wazazi, ndugu na
jamaa zao. Amewaambia waamini kwamba, Kristo ndiye aliyeshinda dhambi na mauti, anayewaalika
waamini kujiachilia mikononi mwake, ili awawezeshe kupata matumaini na ukamilifu wa
maisha!
Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwashukuru wote waliomtumia
salam na matashi mema kwa Siku kuu ya Pasaka na siku ya Jumatano tarehe 23 Aprili
2014 anapofanya kumbu kumbu ya Mtakatifu somo wake. Anawashukuru wote wanaoendelea
kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jumapili ijayo, Jimboni Alba, Kaskazini
mwa Italia, Kanisa litamtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Giuseppe Giroti kuwa Mwenyeheri.
Aliuwawa na Jeshi la Wanazi kutokana na chuki za kiimani. Mfano wa maisha ya Mwenyeheri
Giuseppe Giroti ulete mwamko na ari miongoni mwa waamini kutaka kujishikamanisha na
Kristo pamoja na Injili yake. Ametambua uwepo wa vijana kutoka Jimbo kuu la Milano
ambao wako mjini Roma kwa ajili ya kukiri imani yao kwa miamba ya imani.