Kardinali Thèodoro Adrien Sarr, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal katika
ujumbe wake kwa Kipindi cha Pasaka kwa Mwaka 2014 anasema kwamba: uchu wa mali na
madaraka; matumizi haramu ya dawa za kulevya; ulevi wa kupindukia, ukahaba na ngono
ni kati ya mambo makuu yanayowatumbukiza watu wengi katika biashara ya utumwa mamboleo.
Nyakati za Siku kuu si muda wa kutenda dhambi kwa kujiachia ili kumezwa na malimwengu.
Kardinali
Sarr anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kuishi maisha yanayoongozwa
na kanuni msingi za maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao
ya wengi; umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Anawaalika watu kuondokana na imani
za kishirikina na nguvu za giza zinazowasababishia hofu na mashaka katika maisha;
uchu wa mali na madaraka unaowatumbukiza wengi katika vita na migongano ya kiuchumi
na kijamii.
Pasaka kiwe ni kipindi muafaka cha waamini pamoja na watu wenye
mapenzi mema kujiondoa kabisa katika utumwa mamboleo unaowatmbukiza katika majanga
ya maisha, ukosefu wa haki msingi za binadamu na matokeo yake ni watu kutokomea katika
upweke hasi unaoweza kuwasababishia kifo. Wakristo wanachangamotishwa kuhakikisha
kwamba, wanaziishi katika ukamilifu ahadi zao za Ubatizo, kwa kumpatia Mwenyezi Mungu
kipaumbele cha kwanza sanjari na kupendana wao kwa wao badala ya kuangaliana kwa "macho
ya makengeza".