Hija ya kichungaji ya Papa Francisko, nchini Korea
Maandalizi ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Korea ya Kusini kuanzia
tarehe 14 hadi tarehe 18 Julai 2014 yanayoongozwa na kauli mbiu “Ondoka, uangaze kwa
kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia” sanjari na Siku ya sita ya
Vijana Barani Asia yanaendelea vyema. Itakumbukwa kwamba, Papa Yohane Paulo II alifanya
hija ya kichungaji Korea ya Kusini, yapata miaka ishirini na mitano iliyopita.
Baba Mtakatifu
Francisko anawaalika wananchi wa Korea katika ujumla wao, kusimama kifua mbele kama
mawimbi na kuangaka kama miale ya moto! Hija ya kichungaji pamoja na mambo mengine
ni changamoto ya kudumisha mchakato wa upatanisho kati ya Korea ya Kaskazini na Korea
ya Kusini, ili kweli amani na utulivu viweze kutawala.
Nembo la hija ya hija
hii ya kichungaji inaviashiria vya sadaka kubwa iliyotolewa na Mashahidi 124 wa Korea
waliomimina maisha yao kwa ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa lake kati ya Mwaka
1791 na Mwaka 1888. Kimsingi, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea ya Kusini,
Jimboni Daejeon ni kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya sita ya Vijana Barani Asia,
inayowataka vijana kuondoka na kuangaza, kwani utukufu wa Mashahidi utawang’aria pamoja
na kuwatangaza watumishi wa Mungu 124 kuwa ni Wenyeheri.
Papa Yohane Paulo
II alipotembelea nchini Korea, alipata fursa ya kuwatangaza wenyeheri 103 kuwa ni
Watakatifu na Mashahidi wa Kanisa. Kati yao kuna Mtakatifu Andrea Kim Tae-gon, Padre
wa kwanza mzalendo kutoka Korea. Katika miaka ya hivi karibuni, Kanisa Barani Asia
limeendelea kukua na kuongezeka maradufu, ingawa bado lina idadi ya waamini wachache
ikilinganishwa na dini kubwa Barani Asia.
Kanisa nchini Korea linaendelea
kukua na kupanuka na kwa sasa takwimu zinaonesha kwamba, lina jumla ya waamini wapatao
millioni tano, sawa na asilimia 10% ya idadi ya wananchi wote wa Korea.