2014-04-22 08:25:05

Ujumbe wa AMECEA kwa ajili ya Siku kuu ya Pasaka 2014


Tume ya haki na amani ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA katika ujumbe wake wa Kipindi cha Pasaka inasema kwamba, Nchi za AMECEA zimebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa watu wema, wenye maisha na imani thabiti, lakini wanaoishi kwa wasi wasi kutokana na kulega lega kwa misingi ya haki, amani na utulivu. RealAudioMP3

Sudan ya Kusini, Malawi na Kenya ni kati ya nchi za AMECEA zinazohitaji sala maalum kwani zinakabiliana na changamoto za uchaguzi ambazo mara nyingi zimekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu.

Kunako Mwaka 2011, Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake, ikashangilia sana kama mwanzo wa matumaini mapya, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa takribani miaka arobaini, wanawanchi wa Sudan ya Kusini waliishi katikati ya mtutu wa bunduki, kiasi kwamba, amani na utulivu ulikuwa ni msamihati mgeni kwao.

Miaka arobaini ya vita na mapambano ya wenyewe kwa wenyewe yalisababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu, huduma duni katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya watu pamoja na umaskini mkubwa wa hali na kipato. Inasikitisha kuona kwamba, ndoto ya amani, utulivu na maendeleo inatoweka taratibu na matokeo yake ni vita, umaskini, njaa na maradhi kuanza kushika kasi.

Ni matumaini ya AMECEA kwamba, mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Malawi utakuwa huru, kweli na wazi, ili kudumisha misingi ya amani, utulivu na maendeleo ya wengi. Kunako Mwaka 2009, Malawi ilifanya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu na ikapongezwa na Jumuiya ya Kimataifa, ingawa kulikuwepo na kasoro ambazo zilitaka kuzima mchakato mzima wa demokrasia ya kweli. Hakukuwepo na fursa sawa katika kampeni, hali ambayo ilisababisha baadhi ya makundi kulalamikia hali hii, kiasi cha kuzua kinzani na migongano ya kijamii. Ni matumaini ya AMECEA kwamba, uchaguzi mkuu wa Mwaka 2014 utakuwa huru, kweli na wa haki.

Kenya ni nchi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni inaendelea kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyotishia amani, usalama na utulivu miongoni mwa wananchi wa Kenya. Wananchi wa Kenya wanakiu ya kuona amani na utulivu vinatawala tena, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu. Ndiyo maana AMECEA inawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Kenya.

Amani ni kati ya zawadi kubwa ambayo Yesu Kristo Mfufuka aliwaachia wanafunzi wake. Amani ni tunda la haki na mapendo; ni kikolezo cha maendeleo endelevu; mazingira ambayo yanamwezesha mwanadamu kuishi utimilifu wa maisha. Kuna uhusiano mkubwa kati ya maisha na amani yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha amani na utulivu; umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Pasaka ni kipindi cha kusherehekea amani na utulivu inayobubujika kutoka katika undani wa maisha ya watu. Huu ni mwaliko wa kuelewa maana ya maisha mapya katika Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.