2014-04-22 09:06:55

Mwenyekiti Halmashauri Walei amwaga "Neno"


Salaam za Sikukuu ya Pasaka na matashi mema kutoka kwa Mwenyekiti wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma, Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es Salaam tarehe 20/4/2014.

Wapendwa Taifa la Mungu,
Wana Familia ya BMMH
Tumsifu Yesu Kristo ……….
KRISTO AMEFUFUKA KWELI KWELI………….

Salaam ya Kristo kwa wanafunzi wake baada ya Ufufuko ilikuwa AMANI IWE KWENU
Nami mtumishi wenu nisiyestahili kwa niaba ya Halmashauri ya Walei ninawaalika tushiriki sote salaam hii ya Kristo Mfufuka nikiwatakia Amani yake itawale katika mioyo yenu na katika familia zenu.
HERI YA SIKUKUU YA PASAKA. ALELU………

Baada ya Ijumaa kuu, leo kwa furaha tunasheherekea PASAKA, Hakika sisi sote ni watu wa PASAKA na Haleluya ndio wimbo wetu, HERI YA SIKUKUU YA PASAKA - ALELU-----YAAA.

Taifa la Mungu, Ufufuko wa BWYK uhuishe upya mioyo yetu katika kumtumikia
“TAZAMA NAYAFANYA YOTE KUWA MAPYA” nawaalika tuendelee kustawisha kanisa mahalia kwa kushiriki wote kukamilisha ujenzi wa Jengo la Ofisi yetu ya Parokia. Na vigango kuendelea kukamilisha vipau mbele vyao
Aidha katika mwaka huu wa familia, Kanisa limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, Familia ni kitovu cha Uinjilishaji Mpya. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba na tafakari zake anawahimiza wanandoa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa dhati katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Basi ninawaalika kuitikia mwito huu wa kuzifanya familia zetu kuwa Makanisa madogo ya nyumbani, shule ya amani, na darasa la furaha, haki , upendo na msamaha.
Kwenu ninyi akina Mama, ambao tumepewa dhamana ya kushiriki katika kazi ya uumbaji kwa kutunza zawadi ya maisha, basi tuendelee kuwa waaminifu katika kutimiza wajibu huo mkubwa, Aidha Kristo ameamua kututunza kwanza kwa kushuhudia zawadi ya ufufuko ikiwa pia ni ishara ya kuinuliwa kwetu kutoka katika hali zote za ukandamizaji katika jamii. Tumshukuru na kufurahi, Hakika Bwana ni mshindi. ALELU………

Taifa la Mungu wana Bikira Maria Mama wa Huruma, kama mjuavyo nchi yetu ipo katika mchakato wa kuandika Katiba mpya, niwaalike basi nasi kama sehemu ya watanzania tunaotumwa kutakatifunza malimwengu na kumleta Kristo Mfufuka katika jamii zetu, ushiriki wetu katika kupata Katiba nzuri iliyosheheni utu na uhuru wa kweli wa binadamu, tunu msingi za taifa, mgawanyo sawia wa rasilimali za nchi, utawala bora na maadili ya viongozi. Kazi hii ni kubwa ; ni nyeti na tete, kwani tunashuhudia malumbano makali yanayoendelea katika Bunge Maalum la Katiba, malumbano haya yanatunyima usingizi na kupata hofu ikiwa kweli matumaini ya watanzania yatafikiwa, tunajiuliza. Je, katiba mpya itafuta machozi ya watanzania wengi?

Basi, hii iwe sala yetu kuu kwa KRISTO Mfufuka, tusali, tuwasindikize wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kwa njia ya sala na majitoleo yetu ili Mwenyezi Mungu awaangazie akili zao na kuimarisha utashi wao ili waweze kutekeleza dhamana hii nyeti kwa ajili ya mafao ya watanzania wote hatimaye tupate katiba Mpya ambayo italinda na kudumisha maendeleo ya sasa na kwa ajili ya vizazi vijavyo aidha, katiba itakayoendelea kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Taifa la Mungu, nimalizie kwa kuwaalika kuendelea kuombea siku ya tarehe 27 Aprili 2014, ambapo Mapapa Wenyeheri walioishi nyakati zetu watatangazwa kuwa watakatifu. Hawa ni Papa Yohane wa XXIII na Papa Yohane Paulo wa II. Mababa hawa ni miamba wa Imani waliojitahidi kusoma alama za nyakati kwa kutangaza maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kumwilisha utume na maisha ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Ili kuwaenzi Mababa hawa, kuna haja ya kujikita katika kutafuta kwanza mafao ya wengi, haki, amani na maendeleo; kutetea zawadi ya uhai pamoja na kuwawezesha vijana katika kuwajengea mfumo wa maisha adili na matakatifu kwa njia ya malezi bora ya familia.
Niwashukuru wote kwa kufanikisha Maadhimisho ya Juma kuu na hatimaye Siku kuu ya Pasaka KWAYA, MINISTRANT, WAHUDUMU, WASOMA MASOMO, KAMATI TENDAJI K,P, WAPAMBAJI.NA WAAMINI WOTE. Niwatakie tena heri ya PASAKA, NA MUNGU ATUKIRIMIE SOTE MEMA YAKE. ALELUYA
Ni mimi Mwenyekiti wenu – HW – Parokia
Donesta Gisselle John Byarugaba.









All the contents on this site are copyrighted ©.