Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka
viongozi nchini kuacha kuwatumia wananchi kama chambo cha kufanikisha malengo yao
ya kisiasa na kusababisha migororo na uvunjifu wa amani.
Aidha, Rais Kikwete
amewataka wananchi wa Wilaya ya Karatu wasiige mfano wa Arusha ambako fujo zinazoongozwa
na baadhi ya viongozi zimezorotesha sana uchumi wa mji huo kwa sababu usalama ni kigezo
kikuu cha maendeleo ya uchumi.
Akizungumza wakati anazindua Jengo la Halmashauri
ya Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha, mjini Karatu asubuhi ya leo, Jumanne, Aprili
22, 2014, Rais Kikwete amesema: “Usalama ni jambo muhimu sana na kwa maana hiyo, nawaombeni
msiige kabisa mfano wa Arusha, sote tunajua kimetokea nini kule kwa sababu ya fujo
za kisiasa ambazo zinachochewa na viongozi na hasa Mbunge wa Arusha mjini Bwana Lema,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Mbunge anayo nafasi kubwa kujenga hoja zake ndani
ya Bunge na ndani ya mikutano ya halmashauri. Lakini kwa mbunge kuwachochea wananchi
na kuwachukua na kuwatembeza barabarani ambako wanakumbana na virugu vya polisi siyo
uongozi wa busara hata kidogo.”
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Karatu, Mheshimiwa Lazaro Titus Massey amewaambia wananchi kuwa moja ya mwelekeo mkuu
wa CHADEMA wilayani Karatu ni kushirikiana na Serikali na polisi katika kudumisha
amani. Tunawakaribisha Arusha waje kujifunza kwetu namna ya kudumisha amani. Tunamkaribisha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Bwana John Mongella kuja kujifunza namna ya kurejesha
na kudumisha amani mjini humo.
Tutaendelea kutumia mashine mpya kukusanya kodi
– Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amesema kuwa Mashine za Electroniki za Ukusanyaji Kodi –EFD ni lazima ziendelee
kutumika nchini na ameagiza viongozi wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) kukaa chini
na wadau na watumiaji wa mashine hizo kuzungumza na kutafuta majawabu yanayolalamikiwa
na wadau.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa anajua kuwa yapo maneno mengi kuhusiana
na mashine hizo lakini Serikali haitarudi nyuma katika matumizi ya mashine kwa sababu
dunia nzima inakwenda huko. Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Serikali kuhusu EFD,
Jumanne, Aprili 22, 2014 wakati alipozunguza kwenye sherehe ya uzinduzi wa Ofisi za
TRA mjini Karatu, Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha.
“Najua kuna maneno mengi
kuhusu suala hili. Kwa hiyo maelekezo yangu ni kwamba kaeni chini, myajadili matatizo
yaliyopo na kupata ufumbuzi. Kama ni suala la bei pia linazungumzika lakini tuhajitaji
mfumo huu wa malipo ya kodi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwenye hili
tusirudi nyuma kwa sababu tukifanya hivyo, tutakuwa tunarudi nyuma sana kwa sababu
dunia nzima inaelekea huko na hata majirani zetu wote ama wameanzisha mfumo huo ama
wanajiandaa kuuanzisha.” Rais Kikwete amesisitiza: “Hatuwezi kurejea kwenye mfumo
ule wa kitumia vijirisiti. Mfumo wa sasa unaifanya kazi ya kukusanya kodi kuwa rahisi
kwa Serikali yenyewe na kwa walipa kodi.
Najua watu hawapendi kulipa kodi
lakini hakuna njia ya jinsi ya kuendelea isipokuwa kwa kulipa kodi”. Rais Kikwete
alikuwa katika ziara ya siku moja kukagua shughuli za maendeleo wilayani Karatu, Mkoa
wa Arusha na kesho atafanya ziara kama hiyo ya siku moja katika Wilaya ya Mwanga,
Mkoa wa Kilimanjaro.