Miaka 20 ya uhuru na demokrasia ya kweli Afrika ya Kusini
Wananchi wa Afrika ya Kusini wanaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na
shukrani kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu walipojipatia uhuru na demokrasia
kamili, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Afrika ya Kusini
pasi na chachu ya ubaguzi wa rangi. Haya ni mafanikio ambayo yamegharimu maisha ya
wananchi wengi wa Afrika ya Kusini.
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya
Kusini kwa namna ya pekee, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunganika
pamoja na kusali, hapo tarehe 27 Aprili 2014 kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuwapatia
demokrasia ya kweli katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Wanapenda kumwomba, ili
awasaidie kuimarisha haki, uhuru, upendo na mshikamano wa kitaifa
Wananchi
wa Afrika ya Kusini wamwombe Mwenyezi Mungu, huruma na msamaha kwa mapungufu yote
yaliyojitokeza katika kipindi hiki sanjari na kuomba neema na mapendo ya Mungu kwa
wananchi wote wa Afrika ya Kusini. Wanaposali na kuomba, wananchi pia wajibidishe
zaidi na zaidi katika kukuza na kudumisha uzalendo, umoja na udugu kwa kutekeleza
nyajibu zao kama raia wema, hasa nyakati za uchaguzi, ili kweli Afrika ya Kusini iweze
kupata viongozi wema na waadilifu, watakaosimamia misingi ya ukweli, haki, amani na
mafao ya wengi.