Simameni kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki na amani!
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anasema ujumbe ambao angependa kuipatia Familia
ya Mungu Afrika Mashariki ni kutaka kuwakumbusha kwamba, Pasaka ni kipindi cha mpito
kutoka katika hali duni na kuingia katika hali bora zaidi ya maisha, kama vile Kristo
alivyojinyemnyekeza na kujishusha, akawa binadamu na kujitwalia hali ya utumishi,
akateswa na kufa Msalabani.
Yesu kwa njia
ya utii kwa Baba yake wa mbinguni, Mwenyezi Mungu amemkirimia jina linalopita majina
yote. Kristo ameshinda mauti na kifo, amefufuka ni mtukufu. Hivyo basi, Pasaka ya
Kristo iwe ni Pasaka ya waamini wote kwa kuondokana na uzembe wa maisha ili kuanza
kuzingatia kweli za Kiinjili kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya ukombozi
iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe.
Upya huu wa maisha unapaswa kujikita katika
ushuhuda wa maisha yenye mvuto wa Kimungu, ili watu wamkimbilie Mungu kupata baraka,
faraja na neema zitakazowasaidia kuwa watu wapya kweli kweli!
Naye Askofu Augustino
Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar katika mahojiano na Radio Vatican anasema ujumbe wa
Pasaka kwa Mwaka 2014 ni amani inayobubujika kutoka kwa Kristo aliyeshinda kifo, dhambi
na ubaya, ili kumkirimia mwanadamu mwanga mpya na utimilifu wa maisha ya binadamu.
Ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya amani kwa binadamu wote. Waamini na watu wote wenye
mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa: kulinda, kutetea na kudumisha msingi
ya haki na amani duniani.