2014-04-21 10:11:08

Pasaka ya familia ya Kikristo!


Wapendwa familia ya Mungu katika Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Redio Vatikan inawatakieni nyote heri, baraka na furaha tele kwa sherehe za Pasaka. Tunamwomba Masiha aliyeshinda dhambi, kifo na mauti, adumishe furaha na utukufu wake katika familia zetu na katika mazingira yote ya maisha yetu. RealAudioMP3

Kwa mwangwi wa maandiko matakatifu (Mt.24:1-12), Kristo aliyeshinda mauti hapatikani tena kati ya wafu. (Kwa nafasi hii, kaburi linawakilisha, dhambi na kifo). Kristo ameshinda dhambi na kifo, AMEFUFUKA. Amevuka kutoka mauti kwenda uzima. Na sisi ambao tumejihinisha kwa mfungo mtakatifu wa siku 40, tufufuke pamoja na Kristo. Tunaomba neema hiyo ya ufufuko itusaidie, tuyashinde maisha ya dhambi, ili ‘atakayetutafuta, asitukute tena tukigaagaa katika maisha ya anasa na dhambi na kifo, asitukute tena Kaburini’.

Kama wenzangu walizoea kunikuta katika ulevi wa aina zote na kila aina ya uzembe, basi nimefufuka pamoja na Kristo, sipo huko tena. Kama majirani zetu walizoea kuikuta familia yetu ikiogelea katika magomvi yasiyokoma, madeni mengi kama ukurutu, maisha ya njaa na miayo mirefu ya kila siku, basi TUMEFUFUKA PAMOJA NA KRISTO, hatupo huko tena. Pasaka ya Kristo iwe ni Pasaka yetu pia. Sisi kama Waamini-Kristo, Pasaka yetu iwe ni kuvuka, kuhama, kuruka, kuondoka katika maisha ya dhambi na kuelekea maisha adilifu ya imani thabiti katika Kristo. Kuondoka katika maisha ya ubaridi katika imani, kuelekea katika maisha ya uhai katika imani.

Lakini, tukumbuke kwamba, sisi Wakrito, ni wabeba-Kristo. Tunu za Kristo na za maisha ya Kikristo, haziwezi kubaki tu katika uwanja wa kiroho. Ni vema kujibidisha sana kwa uwezo wetu wote, kuumwilisha Ukristo wetu, yaani kuufanya Ukristo wetu ushikike katika maisha ya kila siku ndani ya jamii tunamoishi. Tunapenda kuwa na Ukristo wa maneno na matendo na siyo tu Ukristo-nadharia tu. Ni katika usambamba huohuo, tunataka kufikiri namna ya kuiweka Pasaka yetu iwe na mashiko katika maisha yetu ya kila siku. Pasaka iwe na mafaa KIROHO NA KIJAMII PIA.

Kisha kutazama kwa uchache yanayohusu Pasaka kwa upande wa kiroho, sasa tuone kwa uchache tena yale yahusuyo jamii. Kama ambavyo kipindi kizima cha mfungo tulikuwa tunashughulikia wongofu wa mwenendo wetu, huku tukijichambua kona zote za maisha yetu, ndivyo tunavyotamani sasa pasaka yetu iwe na mafaa katika nyanja zote za maisha yetu.

Endapo tulikuwa wafu katika mahusiano na majirani zetu, basi sasa tunataka kuzika ule uhasama wote, na tuwe majirani wema tunaoishi kwa amani na watu wote (Ebr.12:14). Chuki, uhasama na magomvi havina nafasi tena kwetu. Endapo tulikuwa wafu kiuchumi kwa sababu ya uzembe wetu, sasa tunataka tuvuke kutoka katika hali ya uvivu na uombaomba, tuweke mipango vizuri ya familia, tufanye kazi kwa moyo, tule kazi ya vidole vyetu(tufufuke kiuchumi). Kama tulikuwa wafu kwa sababu ya vimadeni vidogo-vidogo vingi, basi, tuondoke katika utamaduni huo wa madeni na tabia ya ukopaji-hodari, tujijengee dhana ya kujitegemea. Kama tulikuwa wafu katika suala la furaha katika familia yetu, daima tukatawaliwa na vurugu na kila aina ya magomvi, basi tuvuke tuelekee ng’ambo yenye furaha na maelewano mema.

Pasaka yetu, ni sherehe inayotualika zaidi kupanda kiwango kutoka uduni kwenda kwenye ubora zaidi katika nyanja zote za maisha mema. Hata kama tulikuwa katika wema wa fadhila, tunaalikwa kuongeza bidii zaidi ya maisha hayo ya fadhila, kuelekea ukamilifu zaidi, ili tuwe Wakristo wema zaidi. Mwaliko wa pekee hapa kwa kila mmoja ni huu: kujaribu kuona mabadiliko ya kipasaka katika maisha yetu ya kila siku. Wewe na mimi tuizawadie familia na jamii yetu, MTU MWEMA ANAYEFAA.

Mpendwa msikilizaji, mang’amuzi ya maisha yanaonesha kwamba, kwa wengi wetu ni rahisi zaidi kuishi katika ufu kuliko kuishi katika uzima. Ni kama tunaelekea kupenda zaidi mauti kuliko uzima mpya katika Kristo. Hicho ni kikwazo kwa Pasaka. Tunapendelea maisha ya kaburini zaidi kuliko maisha ya uzima na uhuru wa waana wa Mungu. Hapa tulielewe kaburi kama jumla ya tabia mbaya ambazo kila mmoja wetu anazo. Na kila mtu anajua kaburi lake ni nini na liko wapi. Swali la kipasaka ni hili, wataendelea kukutafuta na kukuta huko kaburini kwako MPAKA LINI?? Tuone kwa uchache mambo ambayo yanaweza kuturudisha kaburini na tukaendelea kuonekana huko makaburini tunaendelea kutoa uvundo wa kifo.

Mosi, kutokuwa tayari kubadilika: Tupo ambao tunafikiri kwamba haiwezekani kabisa kuiacha dhambi. Yaani tumejirafikisha na dhambi kiasi kwamba tunaona ugumu kuiacha!! Huo ni utepetevu katika utashi. Ukitaka, dhambi na aina yoyote ile ya dhambi tunaweza kuiacha. Jiwekee tu mkakati na UTAYARI-MAKINI wa kuiacha dhambi. Usikae tu kwenye dhambi hadi hatari ya kifo ndiyo ikutandike teke. Ondoka mwenyewe ukiwa na akili timamu. Kama hatupo tayari kubadilika, tutaendelea kudumu makaburini na tutanuka daima. FUFUKA KUTOKA KWA WAFU!!

Pili, kung’ang’ania maumivu ya kale: Tupo ambao tumewahi kukosewa vibaya katika historia zetu na pengine hata sisi wenyewe tumewahi kujikosea sana, tukajitendea mambo mabaya kabisa katika maisha. JISAMEHE mwenyewe kwa yale uliyojikosea, halafu TUWASAMEHE NA WOTE WALIOTUKOSEA. Msamaha ni dawa nzuri sana katika maisha. Bila kuwa na roho ya msamaha, utajikuta unajilundikia maumivu yasiyoisha, unajijengea kaburi imara la kukutesa maisha yako yote. Samehe kwa faida yako mwenyewe. Kuendelea kung’ang’ania maumivu ya kale tena kwa kiapo, eti ‘aliyonitendea fulani, mimi sitasahau kamwe’! Sasa unamkomoa nani kwa kutosahau kwako? Huko ni kujiangamiza wewe mwenyewe. Utajinyima uwezo wa kufikiri, uwezo wa kutenda kazi vizuri, utashindwa kula vizuri, utashindwa hata kulala vizuri. Maumivu ya kale ni kaburi baya sana, usitembee nalo hilo!! FUFUKA KUTOKA KWA WAFU!!

Tatu, ni kuwa na dhana potovu juu ya uhalisia wa maisha yetu: Nalo hili ni kaburi baya. Katika maisha daima tunaalikwa kujifahamu katika mazuri na mabaya yetu. Tambua vipaji na uwezo wako, tambua pia mapungufu na udhaifu wako. Hutokea mara nyingi baadhi yetu tukajidhania kuwa ni watu wenye akili nyingi na kuwa na uwezo wa kufanya kila kitu! Matokeo yake tukaparamia hata mambo ambayo kwa kweli hatuyawezi, au tukaanza kudharau kila mtu na kuona wengine wote ni duni na dhaifu wasiofaa kitu. Sisi tu wanadamu, tuna maweza na mapungufu. Tujikubali na tuwe tayari kusaidiwa na wenzetu pia. Kufikiri kuwa wewe ni kila kitu na unajua na kuweza kila kitu, hilo ni kaburi baya sana, anza kulifukia kabla halijakumeza.

Tupo pia wengine wetu wenye kaburi baya zaidi la kufikiri kwamba dhambi zetu na uhovyo wetu unasababishwa na wengine. Huko ni kukwepa wajibu!! Mfano baba wa familia anaweza kusema, tabia yake mbovu ya ulevi inasababishwa na mkewe mwenye kelele nyingi, na mama naye anaweza kusema, tabia yake mbaya ya ukali uliopitiliza na madeni kila mtaa inasababishwa na mumewe mzembe. Na watoto nao wakamalizia ngonjera kwa kusema tabia yao ya wizi na udokozi inasababishwa na wazazi wao wasioelewana.

Mwisho wa siku kila mtu atasema tabia yake binafsi inasababishwa na mwingine. Hilo ni kaburi. Kama tunataka kutoka makaburini mwetu, tuwe tayari kujiwajibisha! Tuone juu ya uwajibikaji wetu kwa matendo yetu sisi wenyewe. Tunaahirisha kipindi chetu kwa kuimarishwa na neno lile lisemalo amka wewe uliyelala, fufuka kutoka kwa wafu, naye kristo atakuangaza. Kutoka Studio za Radio Vatican, ni Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.