2014-04-19 07:16:48

Maisha ni mchaka mchaka, vinginevyo utachakachuliwa!


Daima ni mchakamchaka. Tabia ya watu wa ulimwengu wa leo ni ile ya mchakamchaka. Kila kitu kinaenda kwa kasi. Taarifa zinaenda kwa kasi kwa njia ya pembejeo za mawasiliano ya haraka, barabara nzuri na za mikato, na wenzetu walioendelea ndiyo wana magarimoshi yanayoenda kwa umeme kwa mwendo wa kasi.

Tuna kila kitu tunachokitaka kwa haraka, daima tuko katika mchakamchaka na kiherehere cha kufanya mambo kama vile tuna wasiwasi wa kutofika tunakotaka kufika au kutofanikiwa kufanya kwa wakati wake kile tunachotaka kukifanya. Ama kweli ni mchakamchaka wa maisha. Mtu yupo katika kupiga mbio za maendeleo katika maisha. Mtu anapiga mbio kwa vile hana uhakika wa kuwasili au kufikia juu kijamii au kiuchumi au hata kuwazidi wengine. “Tukimbie wakati wengine wanatembea!”

Hali hii ya mchakamchaka na ya mbiombio ndiyo unayoikuta katika Injili ya leo. Mtakatifu Yohani anaposimulia kuhusu kaburi wazi lililokutwa asubuhi ile ya ufufuko, anawaonesha wahusika wote wa tukio lile wakiwa katika mbiombio na mchakamchaka: Maria Magdalena ndiye mwanakiherehere aliyefungia. Alikurupuka asubuhi sana kungali bado giza kwenda kaburini. Alipolikuta jiwe lililofunika kaburi limeondolewa hapo ndipo ilipoanza patashika ya mchakamchaka. Akaenda mbio kwa wanafunzi. Nao wale wanafunzi Simon Petro na Yohane wakaanza mchakamchaka.

Tunaambiwa wakaondoka mbio wote wawili kwenda kaburini. Yohane akamzidi mbio Petro akafika wa kwanza kaburini. Kulikoni? Yaonekana mbio hizo zilipigwa kutokana na wasiwasi, na kiherehere cha kujua kumetokea kitu gani. Budi ieleweke kwamba katika mazingira kama haya, binadamu anakuwa amepagawa na kitu anachokuwa na uhakika nacho kwamba kinaweza kikatokea. Yaani, kinakuwa ni kituko kipya kabisa anachotegemea kukiona au kukipata, kitu kitakachotokea au kilichoishatokea kabla. Katika mantiki hiyo mtu huwa haweza kutulia au kujidanganya kutulia. Wasiwasi na kiherehere chake ni kutaka kukiona au kukijua ni kitu gani ambacho ni budi kitokee lakini hakijui.

Endapo kwa hawa wanafunzi wawili wangemwona Yesu kuwa si kitu cha maana au si kitu cha kukijali, hapo tungewaona wametulia na kufanya mambo kitulivu. Wangeenda kaburini kitulivu tena kwa ajili ya udadisi tu, siyo zaidi. Injili ya Yohani inatafuta kutuingizia vionjo vya wanafunzi hawa wawili, Petro na Yohani wanaokimbia kwenda kaburini. Nafikiri pengine, kwa wote wawili kuna woga labda kuna kitu siyo kwamba hakikwenda sawa, bali wanaonja kwamba imani yao inalazimika kukua ili kutobaki katika woga wa kumtamani tu Bwana wao aliyekufa na sasa hayuko tena. Mbio yao inadhihirisha imani yao. Siyo imani kama ya yule aliye na uhakika bila wasiwasi, la hasha, vinginevyo wangekuwa wamepoozwa, na kukosa mwelekeo na hivi kuchanganyikiwa na miguu kutetemea. Wangekosa nguvu kabisa ya kukimbia, hivi daima wangekuwa wanajikwakwaa na kuanguka. La hasha, kuna kitu!

Mbio na kiherehere cha Mkristu
Mkristu ni yule anayekimbia, anayepiga mbio katika maisha. Mbio za mkristu siyo zile zitokanazo na kutokuwa na uhakika wa kuwasili au kufikia juu kijamii au kiuchumi au kupiga mbio za kuwazidi wengine, bali anakimbia kwa vile anajisikia kuwa ni muhimu kuonja uwepo wa Mungu katika maisha yake binafsi.

Tunajitambua katika mbio hizi? Tuna wasiwasi hata sisi katika kumwelewa Kristu angalao kidogo Kristu ambaye wakati mwigine tunaamini amekufa na kuzikwa katika maisha na katika maisha ya jamii?

Tunakubaliana na kupokea hatari ya kuanguka na kujikwaa katika mwendo wetu wa imani? Tunasadiki kwamba kuwa na imani kunamaanisha kwenda mbele katika kutafiti na kuhitaji kupanua uelewa wetu wa imani. Au tunatafuta kwa mbinu na gharama zozote zile kutafuta au kubaki mahali pamoja penye kutupatia uhakika na usalama? Kanisa (tuko wote humo ndani) wakati mwingine hupunguza kasi, au mwendo na kutamani au kutulia katika uhakika na usalama wa hali tuliyofikia.

Petro na Yohane, wakiwa wameambukizwa na kasi ya Magdalena wanaanza kukimbia pamoja.
Tuanze hata sisi mchakamchaka wa kumtafuta Yesu, tuwahusishe katika mchakamchaka huo hata wale walio karibu nasi, labda wamezuiwa na matatizo fulani au na harakati za maisha ya leo.

Heri sana kwa Pasaka yenye mbio… ili maisha yasikwame.








All the contents on this site are copyrighted ©.