2014-04-16 09:35:12

Tamko la viongozi wa Makanisa nchini Kenya: ulinzi na usalama!


Viongozi wakuu wa Makanisa nchini Kenya katika tamko lao la pamoja wakati huu wa Juma kuu na hatimaye, Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka wanasikitika kusema kwamba, amani, usalama na utulivu ni mambo ambayo yameendelea kutoweka nchini Kenya kutokana na mashambulizi ya kigaidi, kiasi cha kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu na mali.

Viongozi wa Makanisa wanapongeza mikakati inayofanywa na Serikali ya Kenya, lakini wanalaani baadhi ya viongozi wa ulinzi na usalama ambao wameshindwa kutekeleza wajibu wao kiasi kwamba, leo kuna watu wengi wanaomiliki na kutumia silaha kinyume cha sheria, mambo yanayochochea uvunjifu wa amani na utulivu nchini Kenya. Katika kampeni dhidi ya vitendo vya kigaidi, ujambazi, wizi wa mifugo, ujangiri na ubakaji: utu na heshima ya binanadamu, zawadi ya maisha na haki msingi ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa na vikosi vya ulinzi na usalama.

Viongozi wa Makanisa wanasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya: rushwa na ufisadi; biashara haramu ya silaha na wahamiaji haramu; ongezeko kubwa la umaskini pamoja na ukosefu wa fursa za ajira; kuchangia katika vitendo vya uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu. Serikali haina budi kusimama kidete kulinda na kutetea maisha na mali za wananchi wake na kwamba, wananchi nao wanapaswa kuonesha ushirikiano wa dhati na vyombo vya ulinzi na usalama. Viongozi wa kidini wawe makini na kauli zao, ili zisiwe ni sababu ya kuwagawa na kuwasambaratisha wananchi wa Kenya.

Viongozi wa Makanisa wanasema, baadhi ya shule na taasisi za elimu zimeanza kupoteza dira na mwelekeo na hivyo kuwa ni mahali pa kuunda vijana wenye misimamo mikali, changamoto ya kuangalia kwa umakini mkubwa mfumo wa elimu nchini Kenya kwa kutambua kwamba, Makanisa ni wadau wakuu katika sekta ya elimu.

Ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya na vitendo vya uvunjifu wa amani ni changamoto inayohitaji umakini mkubwa katika kuzuia na kudhibiti vitendo hivi. Viongozi wa kidini hawana budi kushirikishwa kikamilifu ili kwamba, shule na taasisi za elimu ziweze kuendelea kufunda watoto na vijana watakaokuwa ni raia wema na wachamungu.

Viongozi wa Makanisa wanaendelea kusema kwamba, rushwa na ufisadi pamoja na changamoto mbali mbali zinazojionesha katika Katiba Mpya ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza badala ya kutumia muda mrefu kuzungumzia hoja ya kupandisha mishahara, mambo yanayodhihirisha uchu wa mali na madaraka badala ya huduma makini kwa wananchi wa Kenya.

Makanisa katika kipindi hiki cha Juma kuu na hatimaye Pasaka, wanaombea amani, utulivu, mshikamano wa upendo na udugu. Wanawataka Madreva wa vyombo vya moto kuwa makini ili kulinda maisha ya abiria wao. Sherehe za Pasaka ziwe ni chemchemi ya amani ya kudumu, upendo na umoja wa kitaifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.