Malengo ya Maendeleo ya Millenia yaliyokuwa yamebainishwa na Jumuiya ya Kimataifa
ifikapo Mwaka 2015 yalipania pamoja na mambo mengine kuleta mabadiliko makubwa katika
maisha ya watu kwa njia ya mshikamano.
Malengo haya
yalipania kutokomeza baa la njaa na umaskini duniani; kutoa elimu ya msingi kwa wote;
kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano;
kukuza usawa wa kijinsia; kuboresha mazingira sanjari na kupambana na ugonjwa wa Ukimwi
na Malaria duniani.
Kanisa Katoliki kwa njia ya Mashirika yake ya Misaada Kimataifa
na Kitaifa, limekuwa ni kati ya wadau wakuu wanaoshiriki katika mchakato unaopania
kuwaletea watu mabadiliko ya kweli katika maisha yao ya kila siku, kwa kumkomboa mtu
mzima: kiroho na kimwili. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hispania, “Manos Unidas”.
Ni kati ya Mashirika ya Kimataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuendesha
kampeni ya maendeleo kwa ajili ya nchi maskini zaidi duniani.
Kampeni hii
imekuwa ikitekelezwa kwa takribani miaka 55 iliyopita. Mwaka huu, “Manos Unidas” linapenda
kuendeleza mshikamano wa upendo na udugu kama sehemu ya mchakato wa kumletea mwanadamu
maendeleo endelevu kwa kuzingatia: ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni kanuni msingi
katika mchakato wa mabadiliko na maendeleo ya kweli kati ya watu anasema Bwana Soledad
Suarèz, Rais wa Mano Unidas wakati wa uzinduzi wa Kampeni kwa Mwaka 2014. Kiasi cha
Euro Millioni 44. 2 zilikusanywa katika kipindi cha Mwaka 2013, ikiwa ni pungufu ya
kiasi cha Euro millioni 4.
Hiki ni kielelezo cha athari za myumbo wa uchumi
kimataifa. Mano Unidas kuanzia Mwaka 2000 hadi Mwaka 2014 imekuwa ikishiriki kikamilifu
katika Kampeni ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia yaliyopitishwa na
Umoja wa Mataifa, ingawa hadi sasa bado kuna mambo mengi ambayo utekelezaji wake umeyumba
kutokana na sababu mbali mbali. Kuna haja ya kuendelea kudumisha mshikamano wa upendo
na udugu kati ya mataifa kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na matatizo pamoja
na changamoto mbali mbali za maisha ya mwanadamu.
Kampeni hii inalenga pia
kusitisha biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu na heshima
ya binadamu, kwa kuwajengea watu uwezo wa kiuchumi ili kuondokana na kishawishi cha
kutaka kupata fedha kwa njia ya mkato. Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,
wanapewa kipaumbele cha pekee ili kuwasaidia watoto hawa kurudi na kuishi katika familia
zao. Manos Unidas, imechangia kwa kiasi kikubwa maboresho katika sekta ya elimu, afya,
kilimo na maendeleo ya wanawake.
Kardinali Antonio Maria Rouco Varela, Askofu
mkuu wa Jimbo kuu la Madrid anasema, Kampeni ya Manos Unidas inakumbusha kwamba, kila
mtu anahusika katika mchakato wa kuleta mabadiliko katika maisha ya watu kama wadau
wakuu na wala si watazamaji. Manos Unidas inajikita kutekeleza dhamana ya kuleta mabadiliko
katika maisha ya watu kwa kusukumwa na imani kwa Yesu na Kanisa lake. Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.