2014-04-16 11:55:53

Mafuta matakatifu ni kielelezo cha huduma kwa Watu wa Mungu


Askofu Isaac Amani wa Jimbo Katoliki Moshi, Tanzania ameongoza ibada ya Misa ya kubariki mafuta ya Krisma ya Wokovu, Jumanne tarehe 15 Aprili 2014 Ibada ambayo imewahusisha Mapadre wote wanaofanya utume wao Jimbo Katoliki Moshi. Kwenye mahubiri wakati wa ibada hiyo Askofu Amani alisema kwamba ni mila na desturi za Kanisa Katoliki kwa kila Askofu kusheherekea ibada hiyo pamoja na Mapadre wa jimbo lake.

Wakati wa ibada hiyo hubarikiwa mafuta matakatifu ambayo hutumiwa katika kipindi cha mwaka mzima ili kuadhimisha Sakramenti mbalimbali za Kanisa kama vile: Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Alisema Askofu Amani kwamba, mafuta haya matakatifu hutumiwa kuwapaka mapadre kwenye viganja wakati wa upadrisho wao kama alama ya kuwapa uwezo wa kuinua mikono yao na kuwabariki watu wa Mungu. Naye Askofu hupakwa mafuta hayo kichwani wakati wa kutawadhwa kwake kama ishara ya kushiriki ufalme wa Kristo, na kuwa mhudumu wa Watu wa Mungu.
Wakristo pia hupakwa mafuta hayo wakati wa Ubatizo na Kipaimara. Hi ni alama ya muungano wao na Mungu na utume wa kuhudumiana kidugu. Wagonjwa nao hupakwa mafuta matakatifu ambayo huashiria uponyaji.

Askofu Amani aliwashukuru mapadre ambao hutumia mafuta haya kwenye huduma mbalimbali za kiroho, kwa ajili ya Watu wa Mungu. Alisema kwamba ni utume wa kila anayepakwa mafuta haya kutambua kwamba, anao wito wa kipekee kabisa wa kufahamu kwamba ameitwa na kuwekwa wakfu kwa ajili ya kuwahudumia ndugu zake katika Kristo.

Hivyo ni jukumu la kila mwamini kutambua na kuthamini wito huo huku wakielewa kwamba, Roho wa Mungu yu juu yao na kwamba wametumwa kuhubiri Habari Njema ya wokovu kwa watu wote. Hivyo watumie muda na vipaji vyao kwa ajili huduma hii ya Kikuhani.

Askofu Amani amewaonya Wakristo kujihadhari na aina mbalimbali za mafuta yanayotumiwa na matapeli na wahubiri wa uwongo ili kuwahadaa na kuwatega wana wapendwa wa Mungu. Aliutahadharisha umma kuwa watu wengi siku hizi za utandawazi hufanya biashara hata kwa jina la dini na miujiza hasa ya uponyaji. Alisema kwamba mafuta yaliyobarikiwa kwenye ibada hii ndiyo tu yanaweza kutumiwa kwenye ibada za na Liturujia zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki.

Zaidi ya mapadre 170 walihudhuria ibada hiyo ya Misa kwenye Kanisa kuu la Kristo Mfame lililoko mjini Moshi. Kwa kawaida ibada hii hufanyika siku ya Alhamisi kuu. Hata hivyo, Jimbo Katoliki la Moshi limeadhimisha ibada hiyo siku ya Jumanne ili kuwapa fursa Mapadre kuweza kusafiri hadi kwenye Parokia zao ili kuadhimisha ibada za Juma kuu wakiwa wameungana na Waamini wao.

Na
Sr. Bridgita Samba Mwawasi,
Jimbo Katoliki Moshi.








All the contents on this site are copyrighted ©.