2014-04-16 08:23:18

Jitahidini kuwa ni Mapadre wenye mvuto na mashiko kwa ajili ya Watu wa Mungu!


Alhamisi kuu, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya siku ile iliyotangulia kuteswa kwake Yesu Kristo alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti ya Daraja Takatifu la Upadre, akaonesha kwa njia ya mfano wa maisha yake, jinsi ya kuwahudumia watu kwa upendo. RealAudioMP3

Alhamisi kuu asubuhi, Kanisa linaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki mafuta ya Krisma ya Wokovu. Mapadre wanaungana na Maaskofu wao mahalia ili kurudia tena ahadi zao za Kipadre.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, kwa Makanisa mengi nchini Tanzania, si rahisi sana kuadhimisha matukio ya Alhamisi kuu kwa pamoja kutokana na sababu za kijiografia na kichungaji. Kumbe, kwa Majimbo mengi, Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta ya Krisma hufanywa mapema, ili kutoa nafasi kwa Mapadre kurudi Parokini kwao, ili kuendelea na huduma za kichungaji, Juma kuu.

Askofu Ngalalekumtwa anasema kwa namna ya pekee Siku ya Alhamisi kuu, Mapadre wanaalikwa kumtazama na kumtafakari Yesu Kristo aliyejitoa kama Mchungaji na Kiongozi, akaonesha uaminifu, utii na upendo usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Uaminifu wa Kristo uwe ni changamoto ya uaminifu wa Mapadre unaojionesha kwa namna ya pekee katika: upendo, unyofu, unyenyekevu na huruma.

Mapadre wajitahidi kuwa ni watu wenye mvuto si kwa sababu ya kuwapendeza watu, bali kutokana na unyofu wa maisha yao, unaowafanya kuwa kweli ni vyombo kwa waamini kuweza kumkimbilia Mungu na Kristo wake. Mapadre wajitahidi kumtazama Kristo kama mfano na kielelezo cha kuigwa. Watambue kwamba, Yesu ndiye mwalimu na mlezi mkuu wa Mapadre wanaoendeleza huruma takatifu kati ya watu wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.