Usawa, unyofu na mshikamano ni kanuni msingi katika mapambano dhidi ya baa la njaa
duniani
Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya
Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasikitika kusema kwamba, takwimu
zinaonesha kuwa matajiri 85 duniani wanamiliki nusu ya utajiri wote wa dunia, changamoto
kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea mambo
makuu matatu: usawa, unyofu na mshikamano.
Mambo haya
yakizingatiwa kikamilifu kwa kutambua kwamba, binadamu wote wanaunda Familia moja
ya binadamu, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha unaweza kupewa kisogo, ufikapo Mwaka
2025, kama inavyojionesha kwenye Kampeni ya Caritas Internationalis katika kupambana
na baa la njaa duniani. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana,
Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, aliwaomba waamini pamoja na watu wote
wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa na Caritas Internationalis
katika kupambana na baa la njaa duniani.
Kardinali Maradiaga anasema, ikiwa
kama: mali, madaraka na utajiri wa kutupwa kwa baadhi ya watu ungetumika kikamilifu
kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi, leo hii umaskini, ujinga na maradhi yangekuwa
ni mambo yaliyopitwa na wakati. Lakini mambo ni tofauti kabisa, kumbe kuna haja kwa
Jamii kuchunguza dhamiri zao, tayari kubadili mwelekeo kwa kukazia haki, usawa, unyofu
na mshikamani wa upendo na udugu miongoni mwa Watu wa Mataifa, ili asiwepo tena mtu
anayekufa kwa baa la njaa duniani.
Kila mtu anapaswa kujiuliza haki inayotiliwa
mkazo na Baba Mtakatifu Francisko ina maana gani katika maisha ya mtu mmoja mmoja
na Jamii katika ujumla wake? Ni mahali gani ambako haki na usawa vimetoweka katika
maisha ya mwanadamu. Je, ninawezaje kujenga maisha yangu katika fadhila ya unyofu?
Ni nani ninayeona anahitaji zaidi msaada wangu kwa wakati huu.
Kutokana na
tafakari hii ya kina, inawezekana kabisa kwamba, Kampeni ya Caritas Internationalis
dhidi ya baa la njaa duniani inaweza kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa changamoto zinazotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii.
Caritas Internationalis inasema, si haki kabisa kwa watu
millioni 800 kuteseka kwa baa la njaa wakati ambapo kuna baadhi ya watu wanakula na
kusaza bila hata ya kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao wanaokufa
kwa baa la njaa sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja kwa watu kuguswa na mateso
pamoja na mahangaiko ya watu kama anavyokazia Baba Mtaktifu Francisko. Dunia imebahatika
kuwa na rasilimali ya kutosha, jambo la msingi ni kuwa na ugavi bora na sahihi unaozingatia
mafao na maendeleo ya wengi. Watu wanaweza kuwa na maisha manyofu, kwa kuwa na matumizi
ya wastani pamoja na kujenga utamaduni wa kutunza chakula kwa kuzingatia vipaumbele
vya mtu katika maisha.
Kipindi cha Kwaresima na hasa Juma kuu kiwe ni fursa
ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu kati ya watu: kwa kugawana
muda, rasilimali, chakula kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji katika mchakato
wa kupambana na baa la njaa na utapiamlo duniani. Ni muda muafaka wa kushikamana ili
kupambana na umaskini unaoendelea kuwanyanyasa watu zaidi ya billioni 3. 5.
Kila
mtu akipenda anaweza kuchangia katika kupambana na baa la umaskini duniani, anasema
Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Caritas Internationalis katika kuhamasisha
Kampeni ya mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.
Imehaririwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.