2014-04-12 07:34:48

Amepanda Punda na wala si Prado, lakini Yesu anafunika! Wamemkubali!


Katika ulimwengu wa leo suala la maandamano limeshamiri karibu katika kila nchi. Maandamano hayo yanakuwa ya jamii fulani inayodai haki yake, mathalani yanaweza kuwa maandamano ya wanawake wanaodai haki zao za kijinsia, wafanyakazi, wanafunzi, waganga nk.

Maandamano mengine yanakuwa ya kufanya kampeni ya uongozi, na mengine ni ya shamrashamra za sikukuu fulani za kidini au arusi nk. Maandamano yoyote yanakuwa na sehemu mbili maalumu yaani pahala pa kuanzia na pa kumalizikia, sehemu hizo zaweza kuwa hospitalini, shuleni, uwanjani, ikulu au hata kanisani nk.

Leo tutayaona maandamano ya namna yake yanayoendeshwa na Yesu. Maandamano hayo siyo ya kufanya mgomo wa madai ya masilahi toka serikalini, la hasha, bali tungeweza kuuingiza kwenye aina kama vile ya kampeni ya kupigania sera zake za uongozi. Maandamano hayo yalikusanya watu wengi sana, wakiwepo wanafunzi wake, mashabiki wengi na wapambe kibao mpaka mji ukatikisika. Yerusalemu hapakutosha! Mapato yake hata viongozi wa dini na wa serikali walipoyaona maandamano hayo wakataharuki na kuulizana: “Ni nani huyu?”

Maandamano ya leo yalianza pahala palipoitwa Bethfage na yakaishia mjini Yerusalemu tena ndani ya Hekaluni. Humo hekaluni, Yesu anahitimisha maandamano siyo kwa kutoa hotuba refu ya ahadi hewa, hapana, bali kwa kuwashughulikia watu waliokuwa wanachenji hela na kufanya biashara ndogondogo hekaluni, halafu siku ya pili yake anapokuwa na njaa anaulaani mtini usiozaa matunda.

Sasa hebu tupaone kwanza pahala palipoanzia na palipoishia maandamano hayo, yaani Bethfage na Yerusalemu. “Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni.” Bethfage, ipo upande wa Mashariki ya mlima wa Mizeituni, baada tu ya Bethfage kuna mlima wa Mizeituni ambako ukisimama juu yake unaweza kuangalia vizuri sana mji wa Yerusalemu ulio chini yake. Neno hili Bethfage ni muunganiko wa maneno mawili, Beth (Bayet) ni nyumba; na Fage ni matunda ya tini yasiyokomaa. Kwa hiyo Bethfage ni nyumba ya matunda ya tini yasiyokomaa.

Jambo la kushangaza ni kwamba baada ya kuingia Yerusalemu na kuwasambaratisha wafanyabiashara hekaluni, linafuata simulizi la mfano ule ambao unonesha kitu gani Mungu anakitegemea toka kwa Taifa lake, yaani kitendo cha Yesu kwenda kutafuta matunda kwenye mti wa mtini na bila kukuta kitu isipokuwa majani matupu, anaulaani. “Mtini ukanyauka mara.” Tendo lile la Yesu ni mfano hai unaolingana na kile anachokitegemea Mungu toka kwa watu wake kifanyike ndani ya hekalu au katika ibada zao, lakini anakikosa.

Mungu anategemea kupata matunda ya upendo, ya haki, ya kuwajali maskini, wajane, yatima na watoto, wageni, badala yake ndani ya hekalu anakuta majani, yaani, liturjia, nyimbo za kupendeza, madhehebu marefu, chetezo, ubani na mishumaa kwa wingi. Vitu hivi havisemi chochote kile mbele ya Mungu kama havizai matunda. Hivyo siyo sadaka ambazo Mungu anategemea kuziona toka kwa watu, kwake Mungu vitu hivyo ni kama majani tu, au ni kama Bethfage tu (matunda yasiyokomaa).

Baada ya kuona maana ya mandhali ya maandamano, sasa tuwaone wahusika wakuu wa maandamano hayo. Anapofika Bethfage anawaagiza wanafunzi wake wamletee usafiri: “Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao,’” Maagizo haya ni ya muhimu sana na umuhimu wake unaonekana jinsi masimulizi yanavyorudi mara mbili. Mosi, pale anapowaagiza mitume wake: “mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee.” halafu inarudiwa tena inaposemwa. “Wale wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaamuru (kuwafungua), wakamleta yule punda na mwanapunda”. Msisitizo upo katika kuwafungua hao punda na kuwaleta ili waweze kutumika kwa kazi atakayoitaka Yesu waifanye. Endapo maandamano haya ni ya kampeni za uongozi, basi yaonekana siri na sera za uongozi huo zimelala katika Punda hao. Kwa hiyo Punda ndiyo wasanii wakuu wa maandamano ya leo.

Kazi ya wanafunzi waliotumwa ni kuwafungua punda. Wanyama hawa punda wana maana gani katika Biblia? Mfalme wa enzi za Wayahudi aliwastaajabia sana Farasi na wapanda Farasi waliojulikana kuwa hodari kwa kupigana vita. Kwa mfano, tunasikia kuwa askari wa Farao Farasi na wapanda Farasi wao wote waliangamizwa baharini. Hivi hata Wafalme wa kiyahudi walikuwa wanatamani sana kuwa na farasi na wapanda farasi. Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, mfalme Salomoni anaonywa asiongeze idadi ya Farasi, na asiuze ndugu zake kwa Wamisri kwa ajili ya kuwa na Farasi na wapanda Farasi (askari). Kutembea juu ya farasi ni alama ya ukuu, uongozi, utawala, ufalme, utajiri na ufahari. Namna ya usafiri unaonesha hadhi ya mtu.

Siku za leo, tunaweza kupata picha ya magari ya gharama na ya fahari wanayotembelea marais, mawaziri, wabunge, makardinali, maaskofu, matajiri, maofisa, nk Itakuwa ni kichekesho na haiwezekani kabisa kumwona kiongozi wa hadhi kama hizo kusafiri kwa lori la mkaa, kwa Bajaji au kwa bodaboda, au baiskeli nk. Katika kampeni za uongozi wa kisiasa, wagombea wanasafiri kwa magari ya gharama za kutisha, kama vile gari aina ya Prado, VX, Helikopta. Hii ndiyo hadhi yao.

Kumbe, katika maandamano ya kampeni za Yesu, anamchagua Punda jike na mwanapunda kuwa prado ya kuingia nayo rasmi mjini Yerusalemu. Hii ndiyo sera mpya ya utawala na uongozi anaotaka Yesu kuuingiza ulimwenguni. Ni kiongozi pekee anayefanya hivyo. Marko anasema kwamba hakukuwahi kutokea mtu mwingine yeyote yule aliyewahi kumpanda yule Punda kabla: “Mtamwona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado” (Mk. 11:2). Tamko hilo la Marko ni muhimu sana, likimaanisha kwamba, hakujawahi tokea mfalme au rais yeyote yule hapa duniani, aliyewahi kujionesha, katika hali kama hii ya utumishi. Yesu ni mfalme wa kwanza na wa mwisho anayependekeza aina hii mpya ya utawala.

Ili kuelewa vizuri ujumbe tunaoletewa hapa hatuna budi kuangalia mwishoni mwa kitabu cha Mwanzo ambako Yakobo anatoa baraka yake kwa watoto wake kumi na wawili, anapotoa baraka kwa Yuda, ambaye ni mtoto wake wa kwanza na atakayekuwa kiongozi wa kabila la Israeli, anasema: “Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria kati ya miguu yake, hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii. Atafunga punda wake katika mzabibu, na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri.” (Mwanzo 49:10-11). Sisi hapa tuko mbele ya kituko hicho cha Yesu anayemfungua punda na mwanapunda kama rejea ya Yuda, yaani yule ambaye ataingiza sera za uongozi, utawala mpya ambao hautakuwa na mwisho. Sasa amefika yule ambaye ni kiongozi mpya wa taifa.

Yesu anasema: ‘Wafungueni mniletee’ Wasanii wakuu tunaoletewa hapa leo, wanayo tabia ya pekee sana. Mnyama huyu anafugwa na kuthaminiwa na binadamu hasa kutokana na tabia yake ya kufanya kazi. Kutokana na tabia hiyo, mnyama huyu anayo majina mengine mengi sana yanayowakilisha udundaji wake wa kazi, wengine wanamwita, Nsikiri, Kihongo, Daqwai, Mbunda au Punda nk. Ukitaka kumsifia mtu anayefanya kazi sana wanasema: “Anafanya kazi kama kihongo.”

Hivi Punda ni alama ya kazi, utumishi, na uvumilivu, hachoki kamwe, daima yuko tayari kubeba mizigo. Tabia hii ya Punda ndiyo ilimvutia Yesu hadi akamchagua kuwa mfano wa kuigwa na kipeo cha utumishi ambao unawakilishwa katika nafsi ya kila mtu. Sisi tunashangaa tunapomwona Yesu anajilinganisha na Punda. Kumbe, yeye alitaka daima ajioneshe kama mtu wa kutumikia. Kwa hiyo anapoagiza “wafungueni Punda” anamaanisha kuwa, Punda hao walikuwa wamefungwa, na katika hali hiyo ya kufungwa hawawezi kufanya kazi. Ilibidi kwanza wafunguliwe ili waweze kufanya kazi.

Kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya kazi na uwezo wa kutumikia. Tunayo hali hiyo kutokana na kufanana kwetu na Mungu katika upendo. Upendo ni zawadi kwa maisha yetu maana yake ni kuwajali wengine, yaani kutumikia. Ndani yetu sisi tunaye huyu Punda, Kihongo, Nsikiri nk. Kwa hiyo, endapo punda hao ni sisi, basi yabidi tufunguliwe tuwe huru kufanya kazi yaani, kutumikia, kuvumilia, kunyenyekea, kuwa tayari daima... Yaani tunao uwezo wa kutumikia, lakini daima tumejifunga hatutaki kujifungua ili tuwe huru kutumikia, badala yake tunataka daima kutumikiwa.

Yesu anawapa wanafunzi wake kazi: “Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, mtaona Punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee”. Kazi ya wanafunzi ni kuamsha nguvu ya kutumikia iliyo ndani yetu, kuifungua na kumpelekea Yesu.

Yesu anaongeza kusema: “na kama mtu akiwaambia neno, semeni, ‘Bwana ana haja nao’”. Maana yake akitokea mtu fulani anakataza au anaonesha kupinga. Mtu huyo si mwingine bali ni mimi ninayesema: Tafadhali uniache huru, Usimfungue punda aliye ndani mwangu. Lakini Yesu anakuhitaji anasema: “Nina haja nawe,” kwa sababu kwa njia ya ushirikiano wetu, Yesu anaweza kuanzisha utawala wake duniani kwa kishindo, lakini siyo utawala wa kukandamiza, bali wa utumishi, wa upendo, na wa haki. Yesu anahitaji mchango wa kura ya moyo wako kwa kadiri ya uwezo wako yaani ujifungue, uwe huru, ujiruhusu, kuwa na haki na upendo wa kutumikia, kuwa tayari kusaidia wengine kusudi kuunda uongozi mpya.

Nabii Zakaria anasema: “Tazama, (Yerusalemu) mfalme wako anakuja kwako, mpole, naye amepanda Punda, na mwana Punda, mtoto wa Punda.” Nabii anasema, mfalme huyo haendi vitani kama mpanda-farasi, bali amepanda punda ambaye ni kwa ajili ya kazi ya kutumikia. Kwa hiyo mfalme (kiongozi) huyo anakuja kutumikia. Wanyofu ndiyo watakorithi ulimwengu huu mpya.

Baada ya kuipata sera ya Yesu kutokana na aina ya usafiri aliotumia katika kampeni yake, sasa tuwaone waandamaji katika msafara huu wa Yesu. Punda walipowasili, “wanafunzi wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.” Vifaa hivi na matendo ya waandamaji ni muhimu sana katika maandamano haya. Hebu tuyafuatilie.

Tafsiri halisi ya nguo hapa ingekuwa mgolole au shuka, yaani ni nguo ya binafsi inayomsitiri mtu anapoivaa au hata kujifunika anapolala. Kadhalika kwa Myahudi, hiyo ilikuwa ni nguo yake binafsi. Ni sawa na vazi binafsi ambalo mtu huwezi ukalitoa kwa yeyote. Unaweza ukagawa kitu kingine lakini siyo shuka ya kujifunika au mgolole wa kujitanda. Kwa hiyo nguo hizo ni alama ya utu wa mtu, nafsi yake, uwepo wake na kila kitu chake.

Wanafunzi wanaweka au kutandika shuka na migolole yao juu ya Kihongo na mtoto wake, inamaanisha kwamba wao wanayatoa maisha yao na kila kitu ikiwemo utajiri wao, kwa utumishi unaopendekezwa na Yesu kutokana na tabia ya huyo Kihongo. Yesu anaikalia hiyo migololi ya wanafunzi hao kuonesha kuwa wako chini ya utawala ambao Yesu ndiye mfalme wake. Wanakubaliana na uongozi huu pamoja na sera zake. Yesu mwenyewe akiwa mnyofu, mnyenyekevu, mpole na mtii anasafiri juu ya Punda aliye mvumilivu, mfanya kazi, mtumishi tu na anakaa juu ya migololi hii ya wanafunzi. Wamepokea, na kuukubali uupya wa masiha huyu, mtumishi na mleta amani. Ndiyo maana ya kuweka migololi yao juu ya Punda.

Watu wengine wengi pia wanajitokeza kushangilia: Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani: wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.”

Watu hao wanafanya mambo tofauti na wanavyofanya wanafunzi. Wanafunzi wanatandika migololi yao juu ya punda kuonesha kwamba wao ndio wanaoendeleza sera za mtindo huo wa uongozi. Watu wengine kumbe wanatandaza nguo zao njiani au barabarani. Kiutamaduni ilikuwa kwamba, wakati wa kumtawaza kiongozi, watu walikuwa wanatandaza nguo ardhini na kushangilia ikiwa na maana kwamba walikuwa wanakubali kujitoa na kujiweka chini ya uongozi wa huyo mfalme.

Katika nafasi hiyo watu walikuwa wanashabikia na kupiga vigelegele lakini mara nyingi hawakuelewa sera za uongozi huo. Katika kundi la maandamaji wa leo yaonekana kulikuwa na wapambe wengi sana: “Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani, na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza wauti wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarakiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.” Watu hawa wote walikuwa wanamshabikia mfalme huyu lakini pengine kadiri ya sera walizokuwa wanazifikiria wao.

Wanampokea lakini kadiri wanavyoelewa wao aina ya Mfalme wanayemtegemea. Ni tofauti na mitume wanaoweka nguo zao juu ya punda. Hata katika mazingira yetu ya sehemu mbalimbali yaweza kutokea wachache wanaoelewa maana ya utumishi ya kumfuata Yesu na watu wengine wakabaki ni wapambe na mashabiki tu. Watu hao wanakata na matawi ya miti kushangilia.

Kuhusu matawi ya miti, kunakumbushia Sikukuu ya Vibanda. Siku hiyo waliyakata matawi ili kusherekea kumbukumbu ya kukombolewa toka utumwani Misri. Hapa sasa wanakata matawi kuonesha kuwa sasa wanao uhuru kwa sababu Masiha amefika. Lakini Masiha huyo wanayemdhani ni wa aina gani? Hapo tunaona ukweli wa usemi kwamba “katika msafara wa mamba kenge nao hawakosekani.” Watu waliendelea kuimba “Mwana wa Daudi” lakini ni mwana wa Daudi wanayemtegemea wao.

Katika sikukuu hii ya Matawi tunaalikwa kujihoji upya ushirika wetu na Kristu. Endapo tunataka kidhati kuwa washiriki wa ufalme mpya anaotupendekezea Yesu yabidi tumfungue punda aliye ndani mwetu ili kuwa na uwezo wa kupenda ambao Mungu ametupatia. Tuwe Punda, Kihongo au Nsikiri aliyefunguliwa na kukubali kumbeba Kristu, yaani kutumikia kwa upendo.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.