2014-04-11 12:14:56

Jumapili ya Matawi


Mpendwa mwana wa Mungu karibuni katika kipindi cha tafakari tunapoadhimisha Dominika ya Matawi, Dominika ambayo ni mwanzo wa Juma Kuu, Juma la Pasaka. Kabla ya Misa Takatifu daima tunaanza kwa maandamano ambayo ni ishara ukumbusho wa kuingia kwa Yesu Kristu Yerusalemu. RealAudioMP3

Ni ishara ya utukufu kwa Mungu juu mbinguni. Mwaliko ambao Mama Kanisa anatupa ni ule wa kumshangilia Bwana na kuandamana tukimsindikiza kuelekea Yerusalemu. Kwa kawaida yaweza kuonekana tunafanya kumbukumbu tu lakini si hivyo bali tunashika imani na tunamsindikiza na kupata neema zote alizozitoa wakati ule na tunashika njia yetu ya kumfuasa yeye tukielekea Pasaka ya Mbinguni.

Ewe msikilizaji, kwa kawaida tunajua kuwa Kristu aliteswa, akafa na kisha kufufuka, kumbe kwa njia hiyo tunapata tumaini na tunaalikwa kufuata nyayo zake daima mpaka kufa kwetu. Kwa jinsi hiyo njia ya Bwana ni njia yetu sote. Mama Kanisa ametuwekea mateso makali ya Bwana mbele yetu ambayo yaweza kuwa ni tishio na hivi kujenga woga katika safari, hata hivyo hatuogopi maana ikiwa Bwana ambaye hakustahili alivumilia, je sisi ambao twasitahili twaweza kukwepa wajibu huo? Si hilo tu bali pia matunda ya mateso makali ya Bwana tumeona ni wokovu wa ulimwengu.

Bwana anapokaribia kuingia Yerusalemu ili kumalizia njia yake ya mateso anapanda mwanapunda, hii ni ishara ya unyenyekevu, ishara ya kuwa yeye si mfalme wa mabavu bali anayetumia upendo kujibu ubaya wa ulimwengu. Hii haina maana kuwa hana uwezo, bali uwezo wake ni kwa ajili ya wokovu wa watu na si wa mapigano ya kivita.

Watu wote wanatandaza nguo na majani ya mitende wanaimba Hosana Mwana wa Daudi, hili ni shangilio kwa Mungu wa mbinguni, ni kiitikio cha utukufu na ushindi wa Bwana. Kwa hakika ni mwendelezo wa shangilio ambalo malaika walilitoa kwa Mwana wa Mungu alipozaliwa pangoni Betlehemu, (Lk 2:14). Jibu la shangilio hili tumpalo Bwana ni amani yangu nawapa, yaani amani iliyo zawadi kwetu, (Yn 14:27).

Nabii Isaya anapoagua juu ya Masiha anatuwekea Masiha aliye mvumilivu, anayetukanwa anayekubali kupigwa na hata kung’olewa ndevu lakini hajibu mapigo, bali ametulia na kuweka tumaini kwa Mungu wake. Jambo hili linakamilika katika Bwana wetu Yesu Kristo, anapoingia Yerusalemu. Mwinjili Matayo anasema tazama maaskari wa Pilato wanavyomdhihaki Yesu Mkombozi” (Mt. 27:27-31). Kwa jinsi hii Nabii Isaya anamtangaza Masiha mshindwa, mteswa, asiyeua lakini anayehuisha kwa upendo na kuleta wokovu.

Mpendwa msikilizaji, Mtume Paulo anawaonya Wafilipi na kisha kuwaimarisha katika kuiga na kujifunza kwa Bwana. Katika familia ya Wafilipi kuna chuki, ugomvi na fitina na hivi anawapa wosia akisema kila mmoja amthamini mwenzake na kwa kukazia wosia huu anaweka mbele yao Yesu Kristu Masiha aliyejishusha mpaka kuwa mwanadamu na si ubinadamu tu bali hata kuteswa na Warumi! Chukua muda kidogo tafakari na fikiri juu ya upeo wa jambo hili!

Fikirini mtu bilionea akijishusha na kukaa na maskini! Kwa hakika mbele ya ulimwengu atakuwa wa ajabu lakini wa maana zaidi mbele ya Mungu. Kristu kwa umwilisho wake hakupoteza Umungu wake bali ulibaki umejificha na hivi Mungu Baba akamwadhimisha mno kwa unyenyekevu wake. Basi mwaliko kwako ni amani na utulivu daima, na Mungu atakuadhimisha mno!

Katika Injili ya Marko katika historia ya mateso anatuwekea Yesu Kristu asiyejibu ubaya wowote unaoelekezwa kwake au kwa wengine kwa nguvu za kivita bali kwa neno la upendo. Tazama dhihaka ya Yuda Iskariote, tazama Mtume Petro anapotumia upanga kukata sikio la mtu aliye kinyume na Bwana. Yote haya anayajibu kwa utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu akisema, rudisha panga alani!

Katika Injili ya Matayo tunamwona mwinjili akiweka mbele yetu msisitizo wa ukamilifu wa yale yaliyoaguliwa na manabii hapo kale juu ya Masiha, yakwamba atateswa na kisha kufa. Tunasoma hili katika aya ya 24: wakati wa karamu ya mwisho akishatangaza atakayemsaliti anamalizia akisema, “Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama maandiko matakatifu yasemavyo”.

Katika aya ya 56, pale Getsemane wanapomkamata, yeye mwenyewe anasema tena, “lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie, kisha wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia”. Mwinjili Matayo anaweka mkazo katika hili kwa sababu anawaandikia Wayahudi akilenga kuweka vizuri dhana ya Masiha yakwamba tegemeo lao la Masiha mwenye utukufu na nguvu za kivita hayupo, bali mpole na mnyenyekevu wa moyo.

Anawajibu wale wote waliokwazwa na tendo la Masiha kuteswa, akileta hoja ya Agano la Kale ya kwamba ilikwishatangazwa na Manabii kwamba angetendewa hivyo. Mpendwa msikilizaji wewe uko upande gani? Upande wa Masiha mwenye siraha za kivita au mpole na mteswa? Tafakari!

Kwa kukaa katika upande wa Masiha mteswa basi unakubaliana na fundisho la Matayo akinukuu maneno ya Bwana, yaani rudisha panga alani. Jambo hili anaambiwa Mt. Petro, wakati huohuo Bwana mwenyewe anarudisha sikio la aliyekatwa. Masiha anamwambia Mt Petro asitumie upanga kamwe maana atumiaye upanga atakufa kwa upanga. (Mt. 26:52) Katika hili Bwana anatangaza amani na upole wa moyo mbele ya madhulumu. Kumbukeni mafundisho ya Origen katika karne za kwanza: “sisi wakristu hatuchukui mapanga tena, hatujifunzi tena kupigana vita kwa maana kwa njia ya Kristu Yesu tumekuwa watu wa amani”

Tunapata kusikia tu, katika Injili ya Matayo kifo cha Yuda Iskariote 27: 3-10). Yuda ni alama ya wafuasi wa Bwana ambao ni wa muda tu wakitarajia ushindi na mafanikio katika mipango yao na hivi Bwana anapoonesha kushindwa basi hukimbia na kumtafuta bwana mwingine ambaye kwa hakika ni kifo. Yuda anakata tamaa, haoni kwamba Bwana ni huruma upeo, kiasi kwamba angeweza kuomba msamaha kama yule mwizi wa msalabani.

Mpendwa msikilizaji, tukio jingine ambalo tunalikuta katika Injili ya Matayo tu, ni lile la kuwekwa walinzi katika kaburi la Bwana, Mt. 27:62-66) Hawa ni alama ya ushindi wa shetani. Yesu anaonekana kushindwa kabisa, na kupatilizwa katika kaburi. Hata hivyo Mungu ataingilia kati na kuonesha ushindi wa Mwanae wa pekee Mt. 28:4. Walinzi watashtushwa na mwanga mkali wa Pasaka na Bwana ataibuka kidedea akiwa mfufuka na mshindi wa vita dhidi ya shetani.

Mpendwa msikilizaji Mwinjili Matayo pamoja na Wainjili wengine wanatuwekea alama ya kupasuka kwa pazia la hekalu vipande viwili toka juu hadi chini akitaka kutuambia kuwa kwa njia ya kifo cha Bwana mipaka kati yetu na Mungu imeondolewa na si tu kati ya Mungu nasi bali kati yetu sisi kwa sisi. Tangu siku anakufa msalabani wote tu wana wa familia moja ya Mungu.

Mpendwa mwanatafakari ukiyakumbuka mateso ya Bwana na kuyaweka moyoni na kisha kuyaunganisha mateso yako na yake basi Pasaka kwako ni Ufufuko kweli. Ninakualika basi umsindikize Bwana katika Juma hili Kuu kwa furaha na utulivu mkamilifu ili mwisho wa mateso tupate matunda ndiyo uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako toka Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.