Mh. sana Padre Placide Lubamba Ndjibu ateuliwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki
la Kasongo, DRC
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa sana Padre Placide Lubamba Ndjibu, kutoka
katika Shirika la Wamissionari wa Afrika kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kasongo,
DRC. Askofu mteule alizaliwa tarehe 26 Oktoba 1959, Jimboni Lubumbashi. Baada ya masomo
na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 27 Julai 1991.
Hadi kuteuliwa
kwake alikuwa ni Padre mkuu wa Kanda ya Wamissionari wa Afrika inayounganisha nchi
ya Burundi, DRC na Rwanda. Tangu Mwaka 1991 hadi mwaka 1994 alifanya kazi nchini Burkina
Faso. Mwaka 1994 hadi mwaka 1996 akaenda kusomea Uandishi wa Habari Chuo Kikuu cha
Friburg, nchini Uswiss. Kati ya Mwaka 1996 hadi mwaka 1998 alitoa huduma za kuhariri
Gazeti la Wamissionari wa Afrika lijulikanalo kama Vivant Universr huko Ubelgiji.
Askofu
mteule Ndjibu kati ya Mwaka 1998 hadi mwaka 2002 alikuwa anafanya utume wake Parokiani
Manzese, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Mwaka 2002 hadi Mwaka 2007 alikuwa
ni Mhariri mkuu wa jarida la KARIBU linalochapishwa mjini Bukavu.
Mwaka 2007
hadi mwaka 2010 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Bernadetta, Jimbo Katoliki
la Lubumbashi. Kuanzia tarehe 1 Septemba 2010 alikuwa anaishi kwenye Makao Makuu ya
Kanda ya Shirika la Wamissionari wa Afrika kwa ajili ya Burundi, DRC na Rwanda.