Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa Familia katika maisha na utume wake!
Kanisa limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na
familia kwa kutambua kwamba, Familia ni kitovu cha Uinjilishaji Mpya. Baba Mtakatifu
Francisko katika hotuba na tafakari zake anawahimiza wanandoa kuhakikisha kwamba,
wanajenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa dhati katika hija ya maisha
yao ya kila siku.
Anawaalika kutumia maneno ya kawaida tu: Samahani, pole
na asante na unihurumie. Familia zinapaswa kujikita katika maisha ya Sala na Tafakari
ya Neno la Mungu ili kuimarisha kifungo cha Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Bila fadhila
hizi, familia nyingi zitajikuta zinageuka kuwa ni uwanja wa fujo na kinzani za kila
aina!
Baba Mtakatifu Francisko anatambua fika changamoto zinazoendelea kuzikumba
familia nyingi duniani kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, misimamo
na mitazamo tenge juu ya tunu msingi za kijamii na kitamaduni pamoja na ukanimungu;
mambo ambayo yamechangia kumong'onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu.
Licha
ya magumu na changamoto zote hizi, lakini watu wengi bado wana hamu na kiu ya kutaka
kujenga maisha ya ndoa na familia, kushiriki katika ujenzi wa Jumuiya kwani wanatambua
kwamba, kama binadamu wanapaswa kushirikiana na wengine na kwa kuwa wao si kisiwa.
Hii ni njia ya kushinda upweke hasi unaoweza kusababisha majanga katika maisha ya
mwanadamu.
Kwa bahati mbaya nguvu na ujasiri huu kutoka katika undani wa watu
unakumbana na vikwazo na changamoto nyingi kiasi kwamba, baadhi ya watu wanashikwa
na kigugumizi cha kufanya maamuzi magumu na mazito katika hija ya maisha yao. Wanaogopa
kushikamana na wenzi wao wa ndoa hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Hofu hii inarutubishwa
na sera na sheria tenge kuhusu maisha ya ndoa na familia, kwa kutafuta mafao binafsi
na kusahau wajibu wa kijamii na utu wema. Kimsingi kuna upungufu mkubwa wa sera makini
kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Hii ni tafakari ya kina inayotolewa
na Padre Andrea Koprowski, Mkurugenzi wa Vipindi, Radio Vatican anapofanya rejea kuhusu
Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Ajili ya Familia kama sehemu ya mchakato wa
kuzihusisha familia za Kikristo katika maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum
ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.
Padre
Koprowski anasema watu wengi wana kiu na hamu ya kuwa na familia inayosimikwa katika
uhusiano wa dhati kati ya Baba, Mama na Watoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu; wanataka kushiriki katika ujenzi wa Jumuiya. Lakini wasi wasi wao mkubwa ni
ukosefu wa fursa za ajira; ukosefu wa makazi bora na salama kwa familia zao, wana
mashaka ya kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwani hawana uhakika na usalama wa
kesho kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa. Watu kwa sasa wanaishi roho juu juu
kama "mkungu wa ndizi".
Kuna makundi ya watu ndani ya Jamii ambayo yamepoteza
dira na mwelekeo, hayaoni tena umuhimu wa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa
sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; hawataki kushiriki katika wito na dhamana ya maisha
ya ndoa na familia wala kushiriki katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira ambayo
kimsingi ni kazi ya uumbaji. Kundi hili la watu linajikita katika ubinafsi na hali
ya kujitafuta lenyewe; ni watu wanaomezwa mno na malimwengu; ni watu ambao wanataka
sifa na madaraka; wanataka utajiri wa haraka haraka hata kwa gharama ya maisha ya
jirani zao.
Changamoto zote hizi ndizo zilizomsukuma Baba Mtakatifu Francisko
kuitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, kwa Mwaka 2014 ili Mababa
wa Sinodi waweze kuchangia kuhusu hali ya maisha ya ndoa na familia katika Majimbo
yao; familia mintarafu mwono wa kijamii na kitamaduni pamoja na changamoto zinazoendelea
kujitokeza. Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwaka 2015 itaibua mapendekezo
ambayo yatapelekwa kwa Baba Mtakatifu ili aweze kuyaundia mikakati ya shughuli za
kichungaji kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu.
Familia ni mada inayopewa kipaumbele
cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu katika Baraza la Makardinali
lililohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican alisikiliza kwa makini mchango uliotolewa
na Makardinali kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na changamoto
zote. Baba Mtakatifu aliwaambia Makardinali kwamba, Familia ni kiini cha maisha ya
Jamii ya binadamu.
Tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu aliwaumba mwanamke na mwanaume,
ili waweze kuzaa na kuijaza dunia. Tafakari inayofanywa na Mama Kanisa ni kuangalia
uzuri wa maisha ya ndoa na familia; kiini cha imani, furaha na matumaini. Kanisa linaangalia
machungu na mateso yanayojitokeza katika maisha ya ndoa na familia. Familia leo hii
inapuuzwa na kunyanyasika, lakini bado waamini wanatamani kujenga na kudumisha familia
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.
Kanisa linapenda kuangalia mpango
wa Mungu kwa familia ya binadamu, ili kuwasaidia wanandoa na familia kuishi kwa furaha
na matumaini makubwa, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija
ya maisha yao hapa duniani. Kumbe si haba anasema Padre Andrea Koprowski, kwamba,
Baba Mtakatifu Francisko ameandika Barua kwa ajili ya Familia za Kikristo kwa kutambua
umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa.
Imehaririwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.