Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum
ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2014 hapa mjini Vatican,
kwa kuongozwa na kauli mbiu "Changamoto za kichungaji kuhusu familia mintarafu Uinjilishaji"
ameandika barua kwa familia zote duniani ili kukazia dhamana ya Kanisa kuendelea kutangaza
Injili kwa kukabiliana kinaga ubaga na changamoto mpya zinazohusu familia.
Baba
Mtakatifu anasema, maandalizi haya yanawahusu Watu wote wa Mungu kwa kuhakikisha kwamba,
wanashiriki kikamilifu kwa kutoa mawazo pamoja na kusindikiza mchakato mzima kwa njia
ya sala, jambo muhimu sana kutoka kwa familia zote. Sinodi hii ni maalum kwa ajili
ya: wito na utume wa Kanisa na Jamii; matatizo yanayowakabili wanandoa; maisha ya
kifamilia, elimu na malezi kwa watoto; dhamana na utume wa familia katika maisha ya
Kanisa.
Baba Mtakatifu anazialika familia kusali na kumwomba Roho Mtakatifu
ili aweze kuwaangazia Mababa wa Sinodi katika kutekeleza wajibu wao huu nyeti. Sinodi
hii maalum, itafuatiwa tena na Sinodi ya kawaida ya Maaskofu itakayojadili kuhusu
tema ya familia mwaka 2015 sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa itakayofanyika
mwezi septemba, mjini Philadelphia, nchini Marekani.
Baba Mtakatifu anawaalika
wanafamilia pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kufanikisha
matukio haya makuu ndani ya Kanisa, ili liweze kung'amua na kupata mikakati itakayosaidia
familia ili kukabiliana na changamoto kadiri ya mwanga na nguvu ya Kiinjili.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, ameitunga barua hii wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha
Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni. Ni tukio ambalo liliwakutanisha Mzee Simeoni
na Anna kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wakamtambua Yesu kuwa ni Masiha. Mzee Simeoni
akamshukuru Mungu kwa kuwa ameuona wokovu na Anna kwa upande wake akasimulia matendo
makuu ya Mungu licha ya uzee wake.
Inafurahisha kuona kwamba, wazee wawili
na vijana wawili wanakutanishwa na Yesu. Hii inaonesha kwamba, Yesu ana uwezo wa kukutanisha
na kuunganisha vizazi, kwani Yeye ni chemchemi ya upendo inayovuka ubinafsi, upweke
na masikitiko. Baba Mtakatifu anasema, familia katika hija ya maisha yao wanashirikishana
na kumegeana mambo mengi mema: chakula na mapumziko; kazi za nyumbani, starehe, sala,
safari na hija ya maisha ya kiroho pamoja na matendo ya huruma.
Pale panapokosekana
upendo, hapo kutakosekana furaha na kwamba, upendo wa kweli unabubujika kutoka kwa
Kristo kwa njia ya Neno lake ambalo ni mwanga katika mapito ya waamini; anawapatia
Mkate wa maisha ya uzima wa milele, unaowasaidia waamini kupambana na changamoto za
maisha ya kila siku.
Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa familia kwa
kuhimiza kwamba, mchango wao wa sala ni muhimu sana katika Maadhimisho ya Sinodi ya
Maaskofu kuhusu Familia. Anawaomba pia kumwombea ili aweze kuwahudumia Watu wa Mungu
katika ukweli na upendo. Baba Mtakatifu anawaombea ulinzi na tunza kutoka kwa Bikira
Maria na Mtakatifu Yosefu, ili waweze kutembea huku wakiwa wameshikamana katika upendo
na huduma.