2013-09-02 14:54:59

Marehemu Kardinali Medardo Mazombwe kuzikwa Jumanne - Lusaka Zambia


Marehemu Kardinali Medardo Mazombwe, Askofu Mkuu Mstaafu wa Lusaka, aliyefariki dunia Alhamis 29 Agosti 2013, hospitalini mjini Lusaka, atazikwa kwa heshima ya kitaifa , Jumanne 3 Septemba 2013, mjini Lusaka.

Jumapili ujumbe wa Mapadre 30, Masista kadhaa na Mabruda , na Walei wake kwa waume kadhaa, wakiongozwa na Askofu George Lungu wa Jimbo la Chipata, waliusindikiza mwili wa hayati Kardinali Mazombwe hadi Chipata eneo alikozaliwa , ambako ilisomwa Ibada ya Misa ya wafu, katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Anna, majira ya saa tisa za mchana. Na mwili ulibaki huko hadi Jumatatu, kabla ya kurudishwa Lusaka Jumatatu hii. Wakazi wa Chiapata waliweza kutoa heshima zao za mwisho.
Marehemu Kardinali Mazombwe atazikwa Jumanne katika Kanisa kuu la Mtoto Yesu, la mjini Lusaka. Msemaji wa Baraza la Maaskofu Zambia, Padre Paulo Samasumo, ametaarifu.

Ijumaa, Rais Michael Sata wa Zambia, alionyesha masikitiko yake kwa Kanisa Katoliki kuondokewa na kiongozi huyu, aliyemtaja kuwa shupavu na aliyeonyesha uthabiti katika utume wake kama Kasisi na Kiongozi wa Kanisa . Anakumbukwa jinsi alivyo simama kidete, kutetea maskini , hadi kuifanikisha Zambia kufutiwa deni lake la nje, wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 2000.

Cardinali Mazombwe, amefariki akiwa na umri wa miaka 82, na pia Zambia inamheshimu kama mzambia wa kwanza kuteuliwa katika cheo cha Kardinali.










All the contents on this site are copyrighted ©.